Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT WAZALENDO Taifa, Raisa Abdallah, amewataka viongozi wa majimbo kuendelea kuimarisha mapambano ya kisiasa kwa lengo la kuleta mabadiliko, akisema Watanzania wana imani na chama hicho katika kuwakomboa dhidi ya utawala alioudai kuwa hauzingatii haki na sheria.

Bi Raisa alitoa kauli hiyo leo, tarehe 17 Mei 2026, katika Jimbo la Tunguu, Mkoa wa kusini Unguja wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kikatiba wa chama hicho.

Akizungumza katika mkutano huo, alisema kuendelea mbele kwa chama kunahitaji kuimarishwa kwa harakati za kisiasa, ikiwemo kufanya mikutano ya matawi na majimbo, ambayo alieleza kuwa ni mihimili muhimu ya uhai wa chama chochote cha siasa.

“Niwapongeze na niwatie moyo viongozi wa Jimbo la Tunguu kwa kufanya mkutano mkuu ambao ni takwa la katiba yetu. Hii inaonesha kuwa chama chetu bado kipo imara,” alisema Bi Raisa.

Aidha, aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanawatambua wanachama wote wa chama katika maeneo yao ili kurahisisha usimamizi na kuwafikia kwa karibu wakati wote.

Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Organisation, Mafunzo na Uchaguzi, Khamis Ali Salum, aliutaka uongozi wa jimbo hilo kuwatambua wapiga kura wao pamoja na kuongeza juhudi za kuandikisha wanachama wapya, akieleza kuwa ongezeko la wanachama litakiwezesha chama kuwa na nguvu zaidi kuelekea uchaguzi zijazo.