Na Mwandishi Wetu

SERIKALI kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na UN-Habitat katika jitihada za kukuza maendeleo endelevu ya miji, makazi bora na upangaji wa matumizi ya ardhi nchini.

Hatua hiyo imebainishwa tarehe 16 Mei 2026 jijini Baku Azerbaijan kati ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Leonard Akwilapo na Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Habitat, Bi. Anacláudia Rossbach ambapo viongozi hao walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo ya makazi na miji.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ikiwemo upangaji miji, maendeleo ya ardhi, makazi salama na nafuu kwa wananchi pamoja na kuboresha huduma za makazi katika maeneo ya mijini na vijijini.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Dkt. Akwilapo alisema Serikali ya Tanzania inaendelea kuweka mazingira rafiki ya ushirikiano na taasisi za kimataifa ili sekta ya ardhi na makazi iweze kuchangia kikamilifu maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya wananchi.

 “Ushirikiano wetu na UN-Habitat ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora, huduma za msingi na miji inayopangwa kwa kuzingatia maendeleo endelevu,” alisema Dkt. Akwilapo.

Aidha, Waziri Akwilapo alitumia nafasi hiyo kuomba kuharakishwa mchakato wa kufunguliwa ofisi ya UN-Habitat nchini Tanzania ili kuimarisha utekelezaji wa shughuli za shirika hilo hapa nchini.

Tayari Ofisi ya UN HABITAT Tanzania imekwisha andaliwa na Wizira ya Ardhi imeteua wataalam wanne kuwezesha shughuli za ofisi hiyo kuanza kazi nchini na Mhe. Dkt Akwilapo alimkaribisha rasmi kadri ya nafsi yake kuja kufungua ofisi hiyo

‘’ Wizara ya Ardhi imekamilisha maandalizi muhimu ikiwemo uteuzi wa wataalam wanne watakaosaidia kuendesha shughuli za awali za ofisi hiyo mara itakapoanza kazi rasmi’’. alisema

Kwa upande wake, Bi. Rossbach alisema UN-Habitat itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa programu mbalimbali zinazolenga kuboresha makazi ya wananchi, kuendeleza miji salama na himilivu pamoja na kuimarisha upangaji wa matumizi ya ardhi.

Kuhusu kufunguliwa ofisi ya shirika hilo nchini, Bi. Rossbach aliahidi kulifanyia kazi ifikapo mwezi Agosti 2026 na tayari Ofisi yake imekiwsha teua Mtaalam atakaye kuwa msimamizi Mkuu wa Ofisi hiyo.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Rogatus Mativila pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratias Kalimenze.