TABORA
Uongozi wa Soko la Madini Nzega mkoani Tabora umempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuanzisha masoko ya madini nchini, hatua iliyotajwa kuleta mapinduzi makubwa katika biashara ya madini kwa kuongeza uwazi, usalama na ufanisi wa shughuli za kibiashara.
Akizungumza katika Soko la Madini Nzega, Katibu wa Soko hilo na mfanyabiashara wa madini, Revocatus Chungu, amesema kuanzishwa kwa masoko rasmi kumewasaidia wafanyabiashara kupata maeneo salama na yenye utaratibu mzuri wa kufanya biashara, tofauti na hapo awali ambapo walikosa mifumo thabiti na kukumbwa na changamoto ikiwemo utapeli kutoka kwa watu wa kati.
Ameeleza kuwa kupitia masoko hayo, biashara za madini sasa zinafanyika kwa uwazi zaidi, Serikali ikiongeza ukusanyaji wa mapato huku wananchi wanaojishughulisha na sekta hiyo wakinufaika moja kwa moja na shughuli za madini.
Chungu ameongeza kuwa masoko ya madini yamerahisisha taratibu za biashara, kuharakisha huduma kwa wafanyabiashara pamoja na kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi katika maeneo yanayozunguka masoko hayo.
Kwa upande wake, mfanyakazi wa kampuni ya Banjul Limited, Hussein Sadala, ameipongeza Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tabora kwa ushirikiano wanaoutoa kwa wadau wa sekta ya madini, akisema hali hiyo imeongeza uwazi na kurahisisha shughuli za biashara.
Amesema uwepo wa masoko ya madini umeondoa changamoto ya kutafuta wateja kwani wanunuzi na wauzaji sasa hukutana moja kwa moja katika soko rasmi, jambo linaloongeza uaminifu, ushindani wa haki na ufanisi wa biashara ya madini nchini.

