Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, amesema kuwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), linatarajia kuanza safari za ndege kuelekea nchini Urusi mnamo Juni, 2026.
Ameyasema hayo leo Mei 15, 2026 jijini Arusha wakati aliposhiriki katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi linaloendelea jijini humo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Waziri Mahmoud ameeleza kuwa, nchi ya Urusi inapendelea kupata mazao yenye viwango vya hali ya juu kutoka nchini Tanzania lakini huenda ni ngumu wafanyabiashara kukidhi kigezo hicho kutokana na uhaba wa usafiri wa haraka wa kufikisha bidhaa zikiwa na ubora wake.
“Tunalishukuru shirika letu la ndege nchini kwa kukamilisha mikataba yote ambapo ifikapo Juni 2026, safari zitaanza kutoka Tanzania kwenda jijini Moscow na baadaye Saint Petersburg. Wakati ndege hizo zinarudi kutoka kwenye maeneo hayo, tunategemea zitabeba watalii watakaokuja kufanya utalii nchini katika maeneo ya Zanzibar, Kilimanjaro na Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa, shirika hilo litakuwa na ndege itakayobeba mizigo hivyo, ametoa rai kwa wafanyabiashara wanaohitaji kusafirisha bidhaa kwa haraka kutumia usafiri huo.
Ametaja baadhi ya fursa ambazo Tanzania na Urusi wanaweza kushirikiana ikiwemo ujenzi wa viwanda vya mbolea, vifaa vya kilimo, shughuli za ufungashaji, usindikaji na uhifadhi wa bidhaa, TEHAMA pamoja na dawa za binadamu.

