NA: MWANDISHI WETU, PANGANI
Suala la kuwajenga wanafunzi kuwa mahiri katika stadi na ujuzi mbalimbali ndiyo mwelekeo wa Taifa letu katika kuwaandaa wahitimu wenye uwezo wa kuhimili ushindani wa kiuchumi.
Katika Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga, mkazo huo unaendelezwa kwa kasi hasa katika somo la Biashara (Business Studies) ambapo baada ya kusoma kwa nadharia, wanafunzi hufanyia kazi walichojifunza kwa vitendo ili kuwajenga katika kujitegemea.
Katika maboresho ya mtaala yaliyofanywa na serikalia ni pamoja na kuwajengea uwezo wanafunzi kuweza kuanzisha shughuli zao binafsi za kuwaingizia kipato ili wajitegemee hasa baada ya kuhitimu masomo yao. Mwalimu Shija Clement anayefundisha somo la Biashara Funguni Sekondari, anasimamia kikamilifu ujifunzaji huo kwa vitendo.
Mathalani, Mei 15, 2026, amesimamia uandaaji wa vitafunwa kwa mara ya pili, kwa wanafunzi wa kidato cha pili ikiwa ni mwendelezo wa utaratibu wa kuwajengea uwezo wanafunzi kubuni, kuanzisha na kuendeleza shughuli ndogondogo za ujasiriamali za kuwaingiza kipato.
Katika awamu ya pili ya mapishi ya vitafunwa, wanafunzi hao wamepika kachori, ndizi za kachori, sambusa za viazi na choroko, bajia na karanga za mayai, huku kukiwa na vifungashio maalum rafiki wa mazingira vyenye jina la shule.
Katika mkazo wa kinachoendelea kufanyika shuleni hapo, Mwalimu Shija amesema “Mtaala wa elimu yetu umebeba mabadiliko makubwa ambayo hatuna budi kuendana nayo, kwahiyo katika somo la Biashara, pamoja na kusoma maarifa katika vitabu, lakini tunapaswa kuyatafsiri maarifa hayo kwa vitendo, ndiyo maana mara kwa mara nawapa wanafunzi wangu kazi kwa vitendo (project) ili kuwajenga katika uwezo wa kuanzisha shughuli zao binafsi.”
Vilevile, Shija amesema amepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wanafunzi an walimu ambao wamenunua bidhaa zao, hivyo kuwezesha mwendelezo wa uandaaji wa bidhaa zao.
Mwalimu Ibrahim Berenge ni miongoni mwa wateja walionunua vitafunwa hivyo, ambaye amepongeza uandaaji mzuri wenye ubora, na amevitumia vitafunwa hivyo kunywea chai muda wa mapumziko ya asubuhi shuleni hapo.

