Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa akizungumza jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa waandishi wa vyombo vya habari kuhusu biashara ya kaboni yaliyoandaliwa na Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) na kufanyika Jijini Dar es Salaam Mei 15, 2026.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa (katikati waliokaa) akiwa katika picha na Viongozi na Watendaji waandamizi wa Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) muda mfupi baada ya kufungua mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu biashara ya kaboni yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam Mei 15, 2026. Kushoto waliokaa ni Afisa Mtendaji Mkuu wa NCMC, Bi. Kathryn Kigaraba.

Baadhi ya waandishi wa vyombo vya habari nchini wakifuatilia mafunzo kuhusu biashara ya kaboni yaliyoendeshwa na Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) na kufanyika Mei 15, 2026 Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya watumishi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) wakifuatilia mafunzo ya kuhusu biashara ya kaboni yaliyofanyika Mei 15, 2026 Jijini Dar es Salaam na kuratibiwa na NCMC.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Sarah Kibonde akifuatilia mafunzo kuhusu biashara ya kaboni yaliyofanyika Mei 15, 2026 Jijini Dar es Salaam na kuratibiwa Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC).
…………
Waandishi wa Vyombo vya Habari wamehimizwa kuwaelimisha wananchi, jamii na wadau wa hifadhi ya mazingira kuhusu fursa zinazotokana na biashara ya kaboni.
Rai hiyo imetolewa Mei 15, 2026 Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa vyombo vya habari nchini kuhusu biashara ya Kaboni.
Mhe. Kwagilwa amesema Waandishi wa Habari ambao ni daraja muhimu kati ya Serikali na jamii katika kuelimisha umma, hivyo mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa kuripoti kwa usahihi masuala yanayohusu sekta hiyo ambayo inaendelea kukua hapa nchini na duniani kwa ujumla.
“Biashara ya kaboni ni moja ya nyenzo zinazochangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, vilevile, inaunga mkono jitihada za Serikali katika kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi pamoja na utekelezaji wa Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris” amesema Kwagilwa.
Aidha ameeleza mafunzo hayo yatasaidia waandishi wa habari kufahamu dhana ya biashara ya kaboni, utaratibu wa kuanzisha na kusimamia miradi ya kaboni nchini, fursa zinazotokana na biashara hiyo na Sheria, Kanuni na Miongozo inayosimamia sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Kwagilwa ameeleza kuwa Biashara ya kaboni ni moja ya nyenzo muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira kwa kuhamasisha utekelezaji wa miradi endelevu yenye kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.
“Nchini Tanzania, Fursa za biashara ya kaboni zinapatikana katika sekta mbalimbali ikiwemo uhifadhi wa misitu na mazingira ya bahari; matumizi ya nishati safi ya kupikia; usimamizi wa taka katika miji na majiji” amesema Mhe. Kwagilwa.
Naibu Kwagilwa amekitaka Kituo cha Taifa cha Kuratibu Biashara ya Kaboni (NCMC) kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu na msaada wa kitaalamu kwa wadau mbalimbali ili kuongeza ushiriki katika biashara ya kaboni na kutumia fursa hiyo kuchochea maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi nchini.
Ameongeza kuwa Kupitia Programu ya Mageuzi ya Kimkakati ya Mazingira (2026–2030), Serikali inalenga kuimarisha ushiriki wa nchi katika biashara ya kaboni kwa kutekeleza miradi 35 katika sekta mbalimbali na kufikia mapato yasiyopungua Dola bilioni 5 ifikapo mwaka 2030.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kuratibu Biashara ya Kaboni (NCMC), Bi. Kathryn Kigaraba kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191, kituo hicho kina jukumu la kuratibu shughuli zinazohusiana na usimamizi wa gesi joto, biashara ya kaboni na masoko ya kaboni.
Ameongeza kuwa NCMC itaendelea kutekeleza majukumu ya kuratibu kaboni ili nchi na wananchi waweze kunufaika na biashara hiyo.
