……….
Na Happy Lazaro, Arusha .
Zaidi ya Waoneshaji 550 kutoka nchi 14 pamoja na mawakala na waendeshaji wa safari zaidi ya 1,000 kutoka nchi zaidi ya 40 duniani wanatarajiwa kushiriki katika maonesho ya KARIBU -KILIFAIR 2026 yatakayofanyika. kuanzia Juni 4 hadi 7, 2026 katika viwanja vya Magereza Kisongo, mkoani Arusha.
Kama maonesho makubwa zaidi ya utalii Afrika Mashariki, KARIBU-KILIFAIR inaendelea kukua na kuwa jukwaa muhimu linalowakutanisha wataalamu wa utalii, wawekezaji, wapenda safari, pamoja na viongozi wa sekta ya utalii kutoka duniani kote.
Aidha, takribani wageni na wadau wa utalii 15,000 wanatarajiwa kuhudhuria ambapo inaendelea kuthibitisha nafasi ya KARIBU-KILIFAIR kama lango kuu la utalii wa Afrika Mashariki.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha ,Wakurugenzi wa Kilifair Promotion s,Tom Kunkler na Dominic Shoo wamesema kuwa , maonesho haya yalizaliwa kutokana na muungano wa maonesho mawili makubwa ya utalii nchini Tanzania — KARIBU Fair (TATO) na KILIFAIR (Kilifair Promotion) — na sasa yamekuwa maonesho makubwa na yenye ushawishi mkubwa zaidi wa utalii katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kwa mara ya kwanza, tukio la mwaka 2026 litafanyika kwa siku 4 kamili na kupanuka hadi kufikia eneo la maonesho lenye ukubwa wa mita za mraba 47,000.
“Maono yetu siku zote yamejengwa katika viwango vya kimataifa vya maonesho, ubunifu, na mpangilio wenye weledi. Mwaka huu tunafurahia kuanzisha maeneo mapya mbalimbali, ikiwemo “Pan Africa Pavilion” chini ya kampeni ya Jumuiya ya Afrika Mashariki “Visit East Africa – Feel the Vibe”, inayolenga kuonesha uzuri, utofauti na fursa zilizopo katika ukanda huu.”amesema
“Kaulimbiu yetu, “Where business meets wildlife” (Mahali biashara inakutana na wanyamapori), inaendelea kutuongoza. Tanzania ni moja ya maeneo ya kipekee duniani kwa utalii wa mikutano na biashara (MICE), ambapo fursa za biashara zinaunganishwa kwa urahisi na vivutio vya kipekee vya wanyamapori na asili.”
Aidha ameishukuru Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Waziri wake Dr. Ashatu Kijaji, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), TANAPA, na wadau wote wanaoendelea kuunga mkono mafanikio ya tukio hili.
Tunawakaribisha kwa moyo mkunjufu kwenye KARIBU-KILIFAIR 2026 na tunatarajia kushiriki nanyi uzoefu huu usiosahaulika.
Vivutio vya asili na utamaduni vya Tanzania vinatajwa kuwa miongoni mwa bora zaidi duniani. Hivi ni pamoja na tambarare za Serengeti National Park, kreta maarufu ya Ngorongoro Crater, na mlima mrefu zaidi Afrika — Mount Kilimanjaro. Kusini mwa nchi kuna Mikumi National Park, Ruaha National Park na Selous Game Reserve. Vivutio vingine ni pamoja na fukwe nzuri za Dar es Salaam.

