Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema uzinduzi wa programu ya kidijitali ya PRIS App ni hatua muhimu katika kuharakisha safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali kupitia ushirikiano wa serikali na sekta binafsi.

Akizungumza leo Mei 14,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa programu hiyo iliyoandaliwa na Puma Energy Tanzania, Makamba amesema sekta ya nishati ina mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa kwa kuwa ndiyo injini inayowezesha usafirishaji, biashara, viwanda, kilimo pamoja na huduma muhimu kwa wananchi.

Amesema serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji yanayolenga kuongeza ushindani na kuleta manufaa kwa wananchi, huku akiipongeza Puma Energy kwa kuendelea kuwekeza nchini kupitia upanuzi wa vituo vya mafuta, huduma za nishati safi pamoja na ubunifu wa kidijitali.

Makamba amesema PRIS App inaendana moja kwa moja na mkakati wa taifa wa uchumi wa kidijitali wa mwaka 2021/2022 unaolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchumi wa kidijitali katika ukanda wa Afrika Mashariki na kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali kwa wananchi.

Aidha amesema mifumo ya kidijitali kama hiyo itaongeza ujumuishi wa kifedha, kurahisisha huduma kwa wananchi na kusaidia serikali kufikia malengo yake ya matumizi ya nishati safi, ikiwemo kuhakikisha asilimia kubwa ya vyombo vya usafiri vinatumia nishati safi ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, alisema uzinduzi wa PRIS App ni sehemu ya mageuzi makubwa ya kidijitali yanayolenga kuwapa wateja thamani zaidi kupitia huduma za kisasa.

Alisema kupitia programu hiyo, wateja watakaonunua mafuta na bidhaa nyingine katika vituo vya Puma wataweza kukusanya pointi na kuzitumia kupata zawadi na huduma mbalimbali kupitia mtandao wa kampuni hiyo na washirika wake wa biashara.

Fatma alisema Puma Energy Tanzania inaendelea kuwa mshirika mkubwa wa maendeleo ya sekta ya nishati nchini ikiwa na zaidi ya vituo 100 vya huduma, huduma za mafuta ya ndege, gesi ya kupikia pamoja na uwekezaji katika miundombinu ya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG).

Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kampuni hiyo imechangia zaidi ya Sh trilioni 1.4 kupitia kodi na tozo mbalimbali serikalini, hatua aliyosema inaonesha dhamira ya kampuni hiyo katika kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Fatma aliwahimiza Watanzania kuendelea kutumia huduma za Puma Energy huku akisisitiza kuwa kampuni hiyo itaendelea kuja na ubunifu unaolenga kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza thamani kwa wateja wake kupitia huduma za kisasa za kidijitali.