Na OWM – TAMISEMI, Dodoma
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR- MUUUB) imetoa mafunzo kwa viongozi na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM – TAMISEMI) yaliyolenga kuwajengea uwezo katika eneo la usimamizi wa utendaji kazi, ufungamanifu wa Mipango ya Maendeleo ya Kitaifa, Mpango Mkakati wa TAMISEMI na Shughuli za kila siku za Watumishi wa Makao Makuu, Mikoa, Halmashauri na Wadau wote ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mafunzo hayo yametolewa leo jijini Dodoma Mei 14, 2026 na Bw. Oswin Mkinga na Paulo Jorojick wa OR- MUUB ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Mheshimiwa Rais, kwa nyakati tofauti ametuagiza watumishi wa umma viongozi na wasio viongozi kuhakikisha tunawahudumia Watanzania, hivyo Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Juma Selemani Mkomi ametulekeza tuje kuwapa mafunzo yatakayowajengea uwezo kiutendaji ili kuongeza ufanisi na tija katika kuwahudumia wananchi,” amesema Bw. Mkinga.
Akiendelea kutoa mafunzo hayo, Bw. Mkinga amesema kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 35 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Watumishi wa Serikali wanatekeleza majukumu ya Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo mafunzo hayo yamelenga kukuza utendaji kazi unaojali wananchi na maslahi ya taifa kwa jumla.
Aidha, Bw. Mkinga ameongeza kuwa baadhi ya watumishi wa umma katika taasisi zao wanafanya kazi ambazo hazina mchango katika utekelezaji wa malengo ya taasisi zao na taifa, hivyo Mfumo wa e-Utendaji (PEPMIS) unasaidia kubaini mipango isiyofungamana, isiyopimika na ambayo haijibu matarajio ya wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu OWM-TAMISEMI, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Bi. Emma Lyimo amesema mafunzo ya mfumo wa e-Utendaji (PEPMIS) ni muhimu katika kutimiza malengo ya Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, hivyo amewataka watumishi na viongozi waliohudhuria mafunzo hayo kuyazingatia kikamilifu na kwenda kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.

