SEHEMU YA PILI NA YA MWISHO
CP Kavirondo anarejelea maelezo yake kwa msisitizo akisema Hatua hiyo imeendelea kuonesha namna serikali inavyowapa nafasi ya pili wafungwa waliobadilika tabia.
Kamishna Kavirondo anasisitiza kuwa mageuzi hayo yamekuwa na matokeo makubwa katika kuwajenga wafungwa kitaaluma na kiuchumi.
Anasema jumla ya wafungwa 1,109 wamepata mafunzo mbalimbali ya ufundi kupitia VETA, Chuo cha Uhasibu Arusha, Chuo cha Ruanda pamoja na Gereza la Vijana Wami.
Kati yao, wanawake 85 walipata mafunzo ya ujuzi huku vijana 139 wakinufaika na programu hizo za urekebishaji. Aidha, takwimu zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2021 hadi Aprili 2026, jumla ya wafungwa 135,236 waliachiliwa huru nchini ambapo 54,094 walikuwa tayari wamepata ujuzi kabla ya kutoka gerezani.
Waliojirudia kufanya makosa na kurejea magerezani walikuwa 19,692 pekee, jambo linalotafsiriwa kama mafanikio ya programu za urekebishaji pamoja na mafunzo wanayopata wafungwa wanapokuwa gerezani.
Wakili msomi kutoka kampuni ya Wintrust Attorneys and Consultants, Juma Mbwambo, anasema hatua zinazochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan zinaonesha dhamira ya kweli ya kuimarisha haki jinai pamoja na kulinda haki za binadamu nchini.
Mbwambo anasisitiza kuwa adhabu ya kifungo haipaswi kuonekana kama mateso pekee bali ni nafasi ya kumrekebisha mhusika ili aweze kurejea katika jamii akiwa mtu mwema na mwenye mchango chanya. Anabainisha kuwa kuundwa kwa Tume ya Haki Jinai kumesaidia kuleta maboresho makubwa katika mfumo wa utoaji haki nchini.
Anaongeza kuwa maboresho hayo yamegusa maeneo ya dhamana, upelelezi pamoja na usikilizwaji wa mashauri ya jinai kwa wakati.
Aidha, anasema mataifa mengi yaliyoendelea yamefanikiwa kupunguza uhalifu kwa kuwekeza zaidi kwenye elimu, mafunzo ya kazi pamoja na programu za urekebishaji kwa wafungwa.
Anasisitiza kuwa Tanzania nayo imeanza kupiga hatua kubwa katika eneo hilo kupitia mageuzi yanayoendelea kufanywa chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan pamoja na dhamira yake ya kuhakikisha utu wa binadamu unazingatiwa hata kwa wafungwa.
Miongoni mwa walionufaika na mfumo huo mpya wa urekebishaji ni Bw. Mussa Malale, mkazi wa Dodoma na mzaliwa wa Mkoa wa Shinyanga . Malale sasa anafanya kazi ya kufunga mfumo wa viyoyozi (AC) katika mradi mkubwa wa kimkakati wa Uwanja wa Ndege wa Msalato jijini Dodoma.
Anasema aliingia gerezani bila taaluma yoyote baada ya kufungwa kifungo cha miaka 33, lakini akiwa gerezani alijifunza taaluma ya umeme wa majumbani iliyobadilisha maisha yake.
“Nilipoingia gerezani sikuwa na fani yoyote, lakini mpaka sasa nimetoka nikiwa fundi umeme, naweza kufunga AC pamoja na kufanya kazi nyingine za umeme,” anasema Malale.
Anaongeza kuwa licha ya changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kazi na mtaji, bado anaamini mafunzo aliyoyapata gerezani yamemfungulia ukurasa mpya wa maisha. Aidha, anasema anajivunia kushiriki katika mradi mkubwa wa serikali wa Msalato jambo analosema limempa matumaini mapya ya maisha baada ya kutoka gerezani.
Katika simulizi yake yenye kugusa hisia, Malale anasema akiwa gerezani alipoteza wazazi wake wote wawili huku mama yake akifariki mwaka 2017 na baba yake mwaka 2024. Hata hivyo, anasema nguvu kubwa aliyobaki nayo ni familia yake, hasa mke wake aliyemvumilia kwa kipindi chote cha miaka 21 aliyokaa gerezani.
“Mwanamke anayekuvumilia ukiwa kwenye shida hastahili kusahaulika,” anasema Malale kwa hisia, akieleza namna alivyoona thamani ya familia katika kipindi kigumu cha maisha yake.
Naye mke wa Malale anabainisha kuwa maisha yalikuwa magumu tangu mume wake alipofungwa lakini hakukata tamaa wala kuiacha familia yao. Anasema alipambana kuwalea watoto huku akisubiri siku ambayo mume wake angerudi nyumbani baada ya kumaliza kifungo chake.
Anaongeza kuwa kurejea kwa mume wake na kuungana tena kwa familia yao ni jambo analomshukuru Mungu kila siku, huku akieleza kuwa safari yao imekuwa ushahidi kuwa hata waliopitia changamoto kubwa wanaweza kuanza upya na kuishi maisha yenye matumaini.
Katika hatua nyingine, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka mkazo mkubwa katika kufanya mageuzi ya mfumo wa magereza nchini kwa lengo la kujenga jamii yenye haki, usalama pamoja na utu wa binadamu.
Kupitia dira hiyo iliyozinduliwa rasmi mwaka 2025, Serikali inalenga kubadili mfumo wa magereza kutoka kuwa sehemu ya kuadhibu pekee na kuwa vituo vya kurekebisha tabia, kutoa ujuzi pamoja na kuwajengea wafungwa uwezo wa kujitegemea wanaporejea katika jamii.
Kwa mujibu wa dira hiyo, mageuzi ya kisheria na haki yataendelea kuimarishwa ili kuhakikisha mfumo wa haki jinai unakuwa wa kisasa, unaozingatia haki za binadamu pamoja na utu wa wafungwa. Aidha, dira hiyo inaeleza kuwa magereza yatatumika kama vituo vya elimu amali na uzalishaji kwa kuwapatia wafungwa mafunzo mbalimbali ya ufundi pamoja na stadi za kazi.
Kupitia mpango huo, wafungwa wanatarajiwa kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kushiriki shughuli za maendeleo mara baada ya kumaliza vifungo vyao. Katika kuongeza ufanisi wa utendaji, Serikali pia imepanga kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa magereza ili kuongeza ufanisi pamoja na usalama.
Kwa ujumla, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuona magereza yanageuka kuwa vituo vya marekebisho, uzalishaji pamoja na matumaini mapya kwa badala ya kuwa sehemu za kuhifadhi watu pekee.
Ni wazi kuwa tuzo aliyotunukiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kubeba tafsiri kubwa zaidi ya heshima ya kawaida kwani imeakisi falsafa ya uongozi inayoweka mbele ubinadamu, matumaini pamoja na nafasi ya pili kwa waliokosea. Katika mfumo huo mpya wa magereza, wafungwa hawaonekani tena kama watu waliopoteza thamani ya maisha yao, bali kama Watanzania wanaostahili kusaidiwa kurejea katika jamii wakiwa bora zaidi kuliko walivyokuwa awali.
