Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amefanya ziara wilayani Ilala ya kutembelea ujenzi wa barabara ya kivule hadi msongola pamoja na ujenzi wa uwanja Gym khana ambao ni moja ya viwanja vinavyotarajiwa kutumika wakati wa mashindano ya AFCON na kuwataka wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kwa viwango bora huku akiwataka wananchi kuwa watulivu katika kipindi cha mpito cha ujenzi
Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati akikagua ujenzi wa Barabara ya Kitunda hadi Msongola wilayani Ilala inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa baadhi ya maeneo na maeneo mengine kiwango cha zege Chalamila amewatoa shaka wananchi kuwa serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo na amemtaka mkandarasi kufanya kazi ipasavyo ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati na ofisi yake haitosita kuchukua hatua endapo kusuasua kutaendelea
Akiwa kwenye eneo la Msongola njia nne Mkuu wa Mkoa Albert Chalamila amewaeleza wananchi kuwa Rais Dokta Samia amekuwa akitafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo shule, hospitali na barabara kwenye maeneo tofauti nchi nzima hivyo wanapaswa kuendelea kuiunga mkono kwa kulipa kodi ili kuongeza nguvu ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi John Magori amesema ujenzi huo wa barabara ya kitunda kuelekea Msongola uliathiriwa na mvua baada ya barabara kuchimbwa na na mvua kunyesha hivyo amewatoa shaka wananchi kuwa ujenzi huo unasimamiwa vyema na utakamilika kwa viwango na kwa wakati
Baadhi ya wananchi wa Kitunda wamemueleza Mkuu huyo wa Mkoa namna ambavyo kusuasua kwa ujenzi wa barabara hiyo pamoja na kukosa njia mbadala kumewasababishia adha kubwa ikiwemo kuongeza gharama za maisha

