Na Silivia Amandius
Biharamulo, Kagera.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera limethibitisha kutokea kwa ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha basi la abiria na lori, na kusababisha kifo cha mtu mmoja pamoja na kujeruhi watu sita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Brasius Chatanda ajali hiyo ilitokea Mei 12, 2026 majira ya saa 12:10 jioni katika eneo la Kitoka, kata ya Ng’ambo wilayani Biharamulo. Ajali hiyo ilihusisha basi la Kampuni ya Abood lenye namba T 417 EEE aina ya Yutong, lililokuwa likitokea Bukoba kuelekea Dar es Salaam, na lori lenye namba T 895 EGE pamoja na tela T 610 EDA aina ya FAW.
Inadaiwa kuwa dereva wa basi hilo alifanya uzembe kwa kushindwa kuchukua tahadhari wakati akijaribu kulipita lori lililokuwa mbele yake, hali iliyosababisha kugongana uso kwa uso na gari jingine la mizigo, kabla ya kuligonga lori hilo kwa nyuma.
Kutokana na ajali hiyo, kondakta wa basi hilo, Stela Paulo, alifariki dunia papo hapo. Watu sita waliopata majeraha ni pamoja na dereva wa basi Sadick Mohamed Masunga (40), pamoja na abiria wengine akiwemo Deogratius Kagombora Matungwa (56), mkazi wa Kimara Dar es Salaam, Tambwe Boniphace (26) raia wa Congo, Amina Hassan Swedi (29), Helmeth Ephraim Munishi na Zena Rajab Daimu (19) mwanafunzi.
Majeruhi wote walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo kwa matibabu na hali zao zinaendelea kuimarika, na dereva wa basi Hilo akikatwa mguu huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa hospitalini hapo.
Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa madereva wote na watumiaji wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuchukua tahadhari wanapoendesha vyombo vya moto, ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.




