Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa amesema Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) inaendelea kwa kasi na utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), huku vipande mbalimbali vya ujenzi vikionesha mafanikio makubwa.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi bungeni jijini Dodoma leo Jumatano Mei 13, 2026, Profesa Mbarawa amesema hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu, ujenzi wa kipande cha kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro pamoja na kipande cha pili kutoka Morogoro hadi Makutupora umekamilika kwa kiwango kikubwa.

Amesema sambamba na utekelezaji wa mradi huo, TRC inaendelea kutoa huduma za usafiri katika vipande vilivyokamilika, hatua inayowezesha wananchi kuanza kunufaika na maboresho ya sekta ya reli nchini.

Kwa upande wa kipande cha Mwanza hadi Isaka, Waziri huyo amesema ujenzi umefikia asilimia 68.77 na kazi zinaendelea vizuri.

Aidha amesema hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu, ujenzi wa kipande cha tatu kutoka Makutupora hadi Tabora na kipande cha nne kutoka Tabora hadi Isaka unaendelea huku shughuli mbalimbali za utekelezaji zikiendelea katika maeneo hayo.

Profesa Mbarawa amesema baadhi ya vipande vya mradi huo vilikuwa na changamoto zilizochukua muda mrefu kutatuliwa na kusababisha kasi ya utekelezaji kupungua katika hatua za awali.

Hata hivyo amesema Serikali imefanikiwa kupata suluhisho la kukamilisha mradi huo baada ya kupata mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.277, sawa na takribani Shilingi trilioni 3.32.

Hatua hiyo inaendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha miundombinu ya reli nchini kwa lengo la kuongeza ufanisi wa usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.