NA DENIS MLOWE, IRINGA
UZINDUZI wa kampeni za uchaguzi wa ubunge wa Jimbo la Isimani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) umefanyika katika Kijiji cha Itunundu, Kata ya Itunundu, ambapo viongozi mbalimbali wa chama wamewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumpigia kura mgombea wa CCM, Emanuela Mtatifikolo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mohamed Abood, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) Mkoa wa Morogoro na mlezi wa CCM Mkoa wa Iringa, alisema chama kimemteua Mtatifikolo kutokana na uwezo wake wa kufanya kazi, nidhamu na kujituma katika kuwatumikia wananchi wa Isimani. Abood alisema CCM ina imani kubwa naye kwa kuwa anaifahamu Isimani pamoja na changamoto za wananchi wake.
Abood aliongeza kuwa mshikamano ndani ya CCM ni mkubwa, na viongozi pamoja na wanachama wameamua kuungana kuhakikisha chama kinapata ushindi wa kishindo.
Aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kumchagua mgombea huyo.
Kwa upande wake, Mtatifikolo alisema akipewa ridhaa ya kuwa mbunge atasimamia maendeleo ya wananchi kwa kushughulikia changamoto mbalimbali, ikiwemo huduma za maji, miundombinu ya barabara na huduma nyingine muhimu za kijamii.
Aliongeza kuwa ataendelea kuhubiri amani, umoja na mshikamano katika jimbo hilo huku akishirikiana kwa karibu na wananchi kuhakikisha maendeleo yanaongezeka.
Akimalizia, Mtatifikolo aliwashukuru viongozi wa chama na wananchi kwa imani waliomuonyesha. Aliahidi kuendeleza miradi yote iliyoanzishwa na marehemu William Lukuvi pamoja na kuanzisha mingine mipya itakayogusa maisha ya wananchi wa Isimani. Alisema analifahamu vizuri jimbo hilo na changamoto zake, na hivyo atafanya kazi kwa ukaribu na wananchi kutafuta suluhisho la changamoto hizo na kuharakisha maendeleo ya jimbo.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kukipatia ushindi Chama Cha Mapinduzi na kuendeleza juhudi za maendeleo katika Jimbo la Isimani.
Katika mkutano huo, Salim Asas, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, aliungana na Abood kumnadi Mtatifikolo Itunundu Pawaga. Asas aliahidi kumpa ushirikiano mkubwa mgombea huyo katika kuhakikisha anapata ushindi mkubwa kwa ajili ya kusukuma mbele maendeleo ya wananchi wa Isimani.
Alisema anamfahamu Mtatifikolo kutokana na kufanya naye kazi kwa muda mrefu na anaamini uchapakazi wake utawanufaisha wananchi.
Katika hatua nyingine, waliokuwa watia nia wa nafasi ya ubunge ndani ya CCM Jimbo la Isimani wametangaza kumuunga mkono rasmi Mtatifikolo.
Wakiongozwa na Arif Abri, aliyeshika nafasi ya nne katika kura za maoni, walisema wamekubaliana na maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM na wako tayari kushirikiana na mgombea huyo kuhakikisha ushindi wa chama.
Arif Abri alisema kuwa ushindani wa ndani ya chama umeisha na sasa nguvu zote zinaelekezwa katika kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo.
Alisisitiza kuwa watendelea kufanya kazi kwa pamoja katika kampeni na shughuli za kisiasa kwa manufaa ya wananchi wa Isimani.