
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inapenda kutoa ufafanuzi kwa Umma kuhusu taarifa iliyochapishwa katika ukurasa wa Jamii Forums tarehe 12/5/2026 yenye kichwa cha habari: “Tumefanya Kazi JKCI–Dar Group Zaidi ya Miaka 30, Tunaondolewa Bila Kulipwa Kiinua Mgongo, Inauma Sana”.
Ni kweli Wafanyakazi 13 walikuwa waajiriwa wa mikataba katika Hospitali ya JKCI – Dar Group na ajira zao zilifikia mwisho tarehe 30 Aprili, 2026 kwa kukosa sifa za kuajiriwa Serikalini kwani wanakosa sifa za Kielimu yaani elimu ya kidato cha nne.
Taasisi inapenda kufafanua kuwa tarehe 1 Julai, 2025 Serikali ilitoa kibali cha ajira kwa Watumishi 149 waliokuwa wakifanya kazi katika Hospitali ya Dar Group kabla ya hospitali hiyo kukabidhiwa kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tarehe 15 Novemba, 2022.
Kabla ya kukabidhiwa kwa JKCI, wafanyakazi hao walikuwa chini ya Hospitali binafsi ya Tanzania Occupational Health Services (TOHS – Dar Group).
Baada ya kutolewa kwa kibali cha kuwaajiri watumishi wa hospitali hiyo Serikalini na Kutokana na taratibu na kanuni za ajira katika Utumishi wa Umma ulifanyika uhakiki na baadhi ya wafanyakazi hawakuweza kuajiriwa Serikalini kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufikisha umri wa zaidi ya miaka 60 pamoja na kutokuwa na sifa za msingi kielimu zinazohitajika ambazo ni kuanzia Kidato cha nne.
Watumishi wanaolalamika wana elimu ya darasa la saba na baada ya kupewa barua zao za kusitisha mikataba yao ya kazi wafanyakazi hao walielekezwa kufuatilia mafao yao kwa kushirikiana na Ofisi kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii walipokuwa wakichangia kwa utaratibu wa mfuko husika.
Taasisi inawaelekeza wafanyakazi hao ambao mikataba yao ya kazi ilisitishwa wenye changamoto au wanaohitaji ufafanuzi zaidi kuhusu malipo yao kuwasiliana na Utawala kwa ajili ya kupata maelekezo na msaada stahiki.
“Afya ya Moyo Wako ni Jukumu Letu”
Imetolewa na:
Rajabu Hamisi
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
