Na Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe amesema kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua mpya za kuimarisha usimamizi wa taka ngumu nchini baada ya kubainika kuwa sehemu kubwa ya taka zinazozalishwa huishia kubaki kwenye mazingira kutokana na mifumo hafifu ya ukusanyaji.
Huku akibainisha kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa za uchakataji na uteketezaji wa taka ili kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira na kuongeza thamani ya taka zinazozalishwa nchini.
Ameyasema hayo Mei 12, 2026 jijini Dodoma alipokuwa akifungua Mkutano wa Mwaka wa Tathmini ya Utekelezaji wa Afua za Udhibiti wa Taka Ngumu na Usafi wa Miji uliowakutanisha wataalamu wa mazingira, viongozi wa serikali pamoja na wadau wa maendeleo.
Aidha, amebainisha kuwa taka zina uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira na kuongeza kipato kwa wananchi endapo zitachukuliwa kama rasilimali badala ya kuonekana kuwa kero kwa jamii.
Pia ameongeza kuwa Serikali imezitaka halmashauri kuhakikisha mapato yanayotokana na shughuli za udhibiti wa taka yanarudishwa kwenye kuboresha huduma za usafi wa mazingira pamoja na kuimarisha vitengo vya ukusanyaji taka.
Prof. Shemdoe amesema kuwa bado baadhi ya halmashauri nchini hazina maeneo rasmi ya kutupia taka hali inayochangia kuongezeka kwa dampo holela na kuathiri mazingira ya wananchi.
Amesema viongozi wa serikali za mitaa, wilaya na mikoa wanapaswa kusimamia kikamilifu agenda ya usafi wa mazingira ili kudhibiti utupaji holela wa taka kwenye mitaro, barabara na maeneo ya makazi.
Aidha, ameongeza kuwa tabia ya kutupa taka kwenye mifereji ya maji imeendelea kusababisha madhara makubwa ikiwemo mafuriko na kuharibika kwa miundombinu katika baadhi ya maeneo ya miji.
Prof. Shemdoe amesema kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na mataifa rafiki kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto ya taka ngumu nchini.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Mabadiliko ya Tabianchi na Tathmini kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Kanizio Manyika amesema kuwa Tanzania huzalisha zaidi ya tani milioni 17 za taka kila mwaka huku asilimia kubwa ya taka hizo zikibaki kwenye mazingira kutokana na changamoto za ukusanyaji.
Aidha, mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Joseph Birango amesema kuwa mazingira machafu yameendelea kuwa chanzo cha magonjwa mengi yanayoikumba jamii hivyo elimu ya usafi wa mazingira inapaswa kupewa kipaumbele zaidi.
Awali, Mwenyekiti wa Wakuu wa Vitengo vya Udhibiti wa Taka na Usafi wa Mazingira Tanzania Bara, William Mpangala amesema kuwa bado kuna changamoto ya utekelezaji wa baadhi ya maelekezo kuhusu urejeshaji wa mapato ya taka kwenye shughuli za usafi wa mazingira nchini.

