NA DENIS MLOWE,MAFINGA
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Mafinga limefanya kikao chake cha kawaida ambapo hoja kuu zilijikita katika changamoto za miundombinu ya barabara, upatikanaji wa maji safi na huduma ya umeme kwa wananchi.
Katika kikao hicho, Msimamizi wa TARURA Mafinga, Mhandisi Nelson Maganga akijibu maswali mbalimbali ya madiwani alieleza kuwa utekelezaji wa miradi ya barabara unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika kabla ya tarehe 30 Juni katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Alisema maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 yamekamilika na utekelezaji utaanza rasmi Julai mosi.
Alifafanua kuwa halmashauri imeanza kutumia utaratibu mpya wa matengenezo ya barabara kwa kushirikisha vikundi vya wananchi kupitia mfumo wa matengenezo ya barabara wa kijamii (CBRN).
Alisema Mafinga inatarajia kuwa na angalau vikundi vitatu vitakavyofanya kazi ndogo ndogo za matengenezo ya barabara kwa lengo la kutoa ajira na kuboresha miundombinu.
Aidha, alieleza kuwa kipaumbele kimewekwa kwenye barabara korofi na zinazotumiwa zaidi na wananchi, huku baadhi ya barabara mpya zikisubiri kuingizwa kwenye bajeti kupitia utaratibu wa kitaifa wa bodi ya barabara.
Kuhusu barabara ya Changalawe, ilielezwa kuwa mkandarasi ameanza kazi ya kuweka lami baada ya kuchelewa kutokana na mchakato wa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT). Kazi hiyo pamoja na ujenzi wa daraja linalounganisha eneo hilo na shule ya sekondari inatarajiwa kukamilika ndani ya siku chache zijazo.
Katika upande wa huduma ya maji, Meneja huduma wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mafinga (MAWASA), Benson Mutazamba, alisema hadi Machi 26 huduma ya maji imefikia asilimia 67.07, sawa na wananchi zaidi ya 82,000 kati ya wakazi zaidi ya 122,000 wa Mji wa Mafinga.
Alieleza kuwa miradi minne ya maji inaendelea kutekelezwa kupitia programu ya maendeleo ya sekta ya maji, ambayo ikikamilika inatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji safi hadi zaidi ya asilimia 95.
Pia alieleza kuwa mradi mmoja wa majitaka uliokuwa unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) umesimama baada ya mfadhili kujiondoa kutokana na mabadiliko ya sera.
Alibainisha kuwa serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 49 kwa ajili ya miradi ya maji Mafinga, na hadi sasa mamlaka imepokea shilingi bilioni 15.6, sawa na asilimia 32 ya fedha zilizoidhinishwa.
Kwa upande wa huduma ya umeme, Afisa Mahusiano kwa Wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Mafinga, Philemon Kaseka, alieleza kuwa shirika linaendelea na miradi ya kuboresha miundombinu ya umeme ili kuimarisha upatikanaji wa huduma.
Alisema miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa kituo cha kupokea umeme cha Luganga chenye thamani ya shilingi bilioni 2.92, pamoja na ujenzi wa njia mpya za kusafirisha umeme (outgoing feeders) ili kupunguza changamoto za ukatikaji wa umeme.
Alifafanua kuwa baadhi ya kazi za mradi huo zimefikia hatua kubwa ya utekelezaji, huku ujenzi wa njia za umeme kutoka Luganga kwenda maeneo mbalimbali ukiendelea vizuri. Pia alisema mradi wa kutenganisha laini za umeme za mijini na vijijini unaendelea ili kuongeza ufanisi wa huduma.
Aidha, alitaja changamoto zinazoikabili TANESCO kuwa ni pamoja na wizi wa vifaa vya umeme, uharibifu wa nguzo na miti kuangukia miundombinu ya umeme, pamoja na ongezeko la mahitaji ya umeme kutokana na kasi ya ukuaji wa mji wa Mafinga.
Hata hivyo, alieleza kuwa shirika linaendelea kufanya matengenezo ya haraka pindi hitilafu zinapotokea ili kuhakikisha huduma ya umeme inaendelea bila kukatika kwa muda mrefu.
Baadhi ya madiwani walieleza changamoto mbalimbali katika kata zao na kuishauri halmashauri kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan barabara, maji na umeme. Walisema wananchi wanatarajia kuona huduma zikiimarika kwa wakati ili kuboresha maisha yao ya kila siku.
Viongozi wa halmashauri pamoja na wataalamu walihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, wataalamu na wananchi katika kutatua changamoto zilizopo na kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa wakati kulingana na mipango ya serikali.
Wakati huo huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Fidelica Myovella amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi, watendaji na wananchi katika kusimamia na kuongeza mapato ya ndani ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka maelekezo ya wazi kwa mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha zinakusanya na kusimamia mapato kwa ufanisi ili yaweze kurejeshwa katika huduma kwa wananchi.
Alibainisha kuwa mapato ya ndani yanatumika moja kwa moja katika kugharamia miradi ya maendeleo kama ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya shule, sekta ya afya, pamoja na huduma nyingine za kijamii zinazogusa maisha ya wananchi kwa karibu.
“Tunapokusanya mapato haya na kuyasimamia vizuri, tunakuwa tunatekeleza maelekezo ya Serikali Kuu na kwa wakati huohuo tunatatua changamoto za wananchi,” alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha, alieleza kuwa uongozi wa Halmashauri umeendelea kushirikiana na watendaji wa kata na mitaa katika kuhakikisha kila upande unawajibika ipasavyo. Katika juhudi za kuhamasisha utendaji kazi, baadhi ya watendaji wamepewa motisha ya fedha kulingana na makusanyo na utendaji wao, hatua inayolenga kuongeza chachu ya uwajibikaji.
Alisisitiza kuwa hatua hiyo siyo adhabu bali ni njia ya kuhamasisha uwajibikaji na ushindani chanya miongoni mwa watendaji, ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Alitoa wito kwa watendaji wote na wananchi kwa ujumla kuendelea kushirikiana kwa karibu na serikali katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa kasi na kwa ufanisi, kwa maslahi ya jamii yote.

