Kamati imeipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa kuiimarisha Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ikiwemo ujenzi wa maghala makubwa pamoja na juhudi za kupunguza madeni yanayoikabili taasisi hiyo muhimu katika sekta ya afya nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa bungeni, Kamati ilieleza kuwa Serikali imejenga maghala mawili makubwa katika mikoa ya Dodoma na Mtwara kwa gharama ya Shilingi bilioni 42.3 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uwezo wa uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya nchini.
Aidha, Kamati ilisema Serikali imeendelea kupunguza deni la bidhaa za miradi misonge kwa kulipa kiasi cha Shilingi bilioni 50, hatua iliyotajwa kusaidia kuimarisha utendaji wa MSD.
Hata hivyo, Kamati ilieleza kuwa MSD bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa mtaji pamoja na madeni makubwa inayoidai Serikali, hali inayodhoofisha uwezo wake wa kutekeleza majukumu kikamilifu.
Ilielezwa kuwa madeni hayo yamegawanyika katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza linahusu bidhaa zinazotolewa kwa vituo vya kutolea huduma za afya kwa matarajio ya kulipwa baadaye vituo vinapopata fedha, huku kundi la pili likihusu gharama za utunzaji na usambazaji wa bidhaa za miradi misonge.
Kamati ilibainisha kuwa jumla ya madeni yote yanayoidai MSD yanafikia takribani Shilingi bilioni 302.2.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vituo vya kutolea huduma za afya vilivyo chini ya Wizara ya Afya vinadaiwa Shilingi bilioni 46.4, huku vile vilivyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI vikidaiwa Shilingi bilioni 83.1.
Aidha, Serikali inadaiwa Shilingi bilioni 172.7 zinazohusiana na bidhaa za afya za miradi misonge.
Kamati pia ilieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2022/2023, ombi la mtaji wa Shilingi bilioni 300 kwa ajili ya MSD liliwasilishwa kupitia Wizara ya Afya ili kuongeza uwezo wa taasisi hiyo katika uzalishaji, ununuzi, utunzaji na usambazaji wa bidhaa za afya.
Ilifafanuliwa kuwa kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 150 zinahitajika kwa ajili ya ununuzi wa dawa, Shilingi bilioni 110 kwa ajili ya kulipa madeni ya washitiri, Shilingi bilioni 24.1 kwa ajili ya ujenzi wa maghala pamoja na Shilingi bilioni 15.4 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Kamati ilisisitiza kuwa Serikali inapaswa kuipa kipaumbele MSD kwa kuhakikisha mtaji huo unapatikana kwa wakati ili kuiwezesha taasisi hiyo kununua mahitaji yote ya bidhaa za afya bila kusubiri fedha kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Aidha, Kamati ilieleza kuwa utolewaji wa fedha zilizoidhinishwa kwa wakati ni muhimu katika kuhakikisha malengo yaliyowekwa kwa mwaka wa fedha husika yanafikiwa kwa ufanisi.
