SERIKALI inatarajia kuzindua Mpango Mkakati wa Mageuzi kwa Mazingira Endelevu wa mwaka 2026 hadi 2030 utakaolenga kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuimarisha usimamizi wa mazingira nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamadi Yussuf Masauni alisema jijini Dar es Salaam kuwa mpango huo ni sehemu ya mageuzi mapana ya sekta ya mazingira yanayolenga kushughulikia changamoto mbalimbali ikiwemo usimamizi duni wa taka ngumu mijini, matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali pamoja na uharibifu wa mazingira.
Masauni alisema mkakati huo utakuwa mfumo wa kitaifa wa mwongozo utakaoratibu hatua za kimazingira kwa kipindi cha miaka mitano, ukiweka mkazo katika uendelevu, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi pamoja na mageuzi ya uchumi wa kijani.
Alisema utekelezaji wa mpango huo utahakikisha uratibu wa pamoja katika sekta muhimu za uchumi zikiwemo kilimo, nishati, viwanda pamoja na maendeleo ya mijini ili kuhakikisha agenda ya mazingira inaingizwa kikamilifu katika mipango ya maendeleo ya taifa.
Aidha, Masauni alieleza kuongezeka kwa umuhimu wa sekta ya kaboni nchini, akibainisha kuwa Serikali inaendelea kuimarisha Kituo cha Kitaifa cha Biashara ya Kaboni ambacho sasa kinafanya kazi kama taasisi huru ya kimkakati.
Alisema kituo hicho kinatarajiwa kuwa chachu ya kuiwezesha Tanzania kunufaika na soko la kimataifa la kaboni pamoja na kufungua fursa za fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Kituo chetu cha Kaboni sasa kina uongozi kamili, bodi ya wakurugenzi, watumishi pamoja na ofisi ya kudumu eneo la Mtumba jijini Dodoma,” alisema Masauni.
Aliongeza kuwa Serikali tayari imeweka kanuni za biashara ya kaboni zilizoanzishwa mwaka 2022 na kufanyiwa maboresho mwaka 2023, ambazo sasa zinatumika kikamilifu kusimamia shughuli za soko la kaboni nchini.
Aidha, Serikali imetenga shilingi bilioni tano kama fedha za awali kwa ajili ya kuanzisha mifumo na miundombinu muhimu ya kituo hicho.
Waziri huyo alisema mpango huo utajumuisha pia maeneo muhimu ya kimazingira ikiwemo upandaji miti kwa wingi, usimamizi endelevu wa mifugo, uboreshaji wa mifumo ya usimamizi wa taka pamoja na udhibiti wa taka za plastiki.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Richard Muyungi alisema wizara inaendelea kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa mageuzi hayo ili kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na fursa za soko la kaboni pamoja na uhifadhi wa mazingira.
Muyungi alisema wizara inaendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti, usimamizi na uratibu wa miradi ya kaboni ili kuongeza mapato ya taifa sambamba na kuunga mkono ajenda ya maendeleo endelevu.
Alisema Serikali inalenga kuiweka Tanzania miongoni mwa nchi zinazoongoza Afrika katika sekta ya kaboni kupitia mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu inayolenga kuongeza tija ya kiuchumi huku ikilinda mazingira.
Serikali inatarajia kuzindua rasmi mpango huo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yatakayofanyika Juni 5, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

