Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) itaendelea kuhakikisha dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine za afya zinazozalishwa nchini zinakidhi viwango vya ubora, usalama na ufanisi ili kulinda afya za wananchi na kuimarisha sekta ya viwanda vya bidhaa tiba nchini.

Waziri Mchengerwa amesema hayo leo Mei 11, 2026 wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/27 Bungeni jijini Dodoma. Amesema TMDA pia imejipanga kutoa msaada wa kiufundi kwa wazalishaji wa ndani ili kuwezesha viwanda vya dawa na vifaa tiba kukidhi vigezo na viwango vya uzalishaji wa bidhaa tiba vinavyotakiwa kitaifa na kimataifa.

Hatua hiyo inaenda sambamba na mkakati wa Serikali wa kuimarisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya ambapo Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) itaendelea kununua dawa zinazozalishwa na wawekezaji wa ndani ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi. “Serikali imejipanga kuhakikisha MSD inanunua kwanza dawa zinazozalishwa ndani ya nchi zilizokidhi viwango vya TMDA kabla ya kwenda kununua kutoka nje ya nchi. Hatua hii inalenga kukuza viwanda vya ndani, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa Taifa,” amesema Waziri Mchengerwa.

Pia amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya, dawa salama na huduma zenye ubora bila kumuacha mtu nyuma.