Wenyeviti wa vyama vya msingi vya ushirika(Amcos)wilayani Mbinga wakimsikiliza mjumbe wa bodi ya kahawa Tanzania Faraja Komba(hayupo pichani)wakati wa mkutano wa bodi ya kahawa Tanzania uliofanyika katika okukumbi wa kanisa katoliki jimbo la Mbinga.

Wadau wa zao la kahawa kutoka kampuni ya Aviv Tanzania Ltd,wakifuatilia mkutano wa wadau wa kahawa kanda ya Ruvuma  katika ukumbi wa kanisa katoliki jimbo la Mbinga.

Meneja wa bodi ya kahawa Tanzania kanda ya Ruvuma Rashid Abilah,akitoa taarifa ya maendeleo ya zao la kahawa kwenye mkutano wa wadau wa zao hilo  jana.

…………..

Na Mwandishi wetu, Mbinga

SERIKALI kupitia bodi ya kahawa Tanzania(TCB)imesema,itawachukulia hatua kali viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika na wafanyabiashara wa kahawa watakaochezea mizani kwa lengo la kuwaibia wakulima wanaponunua kahawa.

Kauli hiyo imetolewa jana na mkurugenzi wa uzalishaji na maendeleo ya zao la kahawa nchini Kajiru Kisenge,wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) na chama kikuu cha ushirika wilaya ya Mbinga (Mbifacu) kwenye mkutano wa wadau wa kahawa kanda ya Ruvuma.

Kisenge alisema,Bodi ya kahawa Tanzania haitavumilia vitendo vya unyonyaji dhidi ya wakulima kwani Serikali kupitia wizara ya kilimo imekuwa inafanya jitihada kubwa kuwasaidia wakulima kupitia vyama vya msingi(Amcos) ili kuhakikisha wanazalisha wakulima wanazalisha kahawa bora.

“Tutawachukulia hatua viongozi wa Amcos na wafanyabiashara wa kahawa wanaochezea mizani,lengo tunataka kukomesha vitendo vya kihuni dhidi ya wakulima wetu kwa sababu tabia hii inarudisha nyuma juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yetu  kwa ajili ya kuwasaidia wakulima ”alisema Kisenge.

Aidha Kisenge,amekitka chama kikuu cha ushirika wa kahawa wilayani Mbinga(Mbifacu)kuzisimamia Amcos zake ili kila chama kiwe na mizani ya Kidijitali kwa ajili ya kupima kahawa mara msimu utakapofunguliwa mwezi Julai mwaka huu.

Kwa upande wake Meneja wa  Mbifacu Faraja Komba,amewaagiza viongozi wa Amcos kurudisha mizani za zamani kwenye ofisi za chama kikuu cha ushirika na  kuwataka kuendelea kutumia mizani mpya za kidijitali  zilizokaguliwa.

Komba,amewatoa hofu wakulima kuhusu upatikanaji wa vifungashio ambapo alisema,katika msimu 2026/2027 chama kikuu kitasambaza vifungashio ususani magunia kama wazabuni watashindwa kusambaza kwa wakati ili kuepusha wakulima kuchelewa kukusanya na kuuza kahawa yao.

Komba ambaye ni mjumbe wa bodi ya kahawa Tanzania,amewasisitiza maafisa ugani kusimamia  suala la ubora wa kahawa inayolimwa kwenye maeneo yao badala ya kuichia serikali kwani  wameajiriwa ili kuwasaidia wakulima kilimo cha kisasa ili waweze kuongeza uzalshaji na kupata kahawa bora.

“Kila mdau atimize wajibu wake,halmashauri ina maafisa ugani wengi kila kata hawa wakisimamia vizuri wakulima watazalisha kahawa  nyingi,safi na bora”alisema Komba.

Katika hatua nyingine,Komba amewaonya viongozi wa Amcos,kutowapokea wageni wanaotoka nje ya nchi wanaokwenda kwenye vyama vyao bila kuripoti ofisi za uhamiaji kwa ajili ya utambuzi na kupata vibali vya kununua kahawa.

Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa bodi ya kahawa Tanzania meneja wa bodi ya kahawa kanda ya Ruvuma Rashid Abilah alisema,ufunguzi wa  msimu mpya wa masoko ya utaanza tarehe 1 Julai na wakulima wadogo watauza kahawa yao kupitia Amcos zilizopo kwenye maeneo yao.

Alisema,vyama vikuu vya ushirika vina wajibu wa kuratibu taarifa za makusanyo na utoaji wa huduma nyingine zitakazokubaliwa huku akiwataka wakurugenzi wa halmashauri zinazolima kahawa kutoa vibali  vya ununuzi kwa wafanyabiashara wenye nia ya kununua kahawa kwenye halmashauri zao.

Rashid alisema,katika msimu 2026/2027 wanatarajia kuzalishaji tani 29,000 za kahawa ikilinganishwa na tani 26,301.86 msimu 2025/2026.