Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa akijibu maswali katika kikao cha Bunge bungeni jijini Dodoma leo Mei 11, 2026.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa akizungumza na Mbunge wa Jimbo la Katavi Mhe. Thomas Kampala wakati wa kikao cha Bunge bungeni jijini Dodoma leo Mei 11, 2026.

…………

Serikali inakamilisha ufungaji wa mfumo wa kisasa wa ufuatiliaji wa uchafuzi wa mazingira utakaowezesha kufuatilia viwango vya uchafuzi kwa wakati na kuchukua hatua za haraka dhidi ya wanaokiuka Sheria.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo Mei 11, 2026.

Alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Temeke Mhe. Mariam Kisangi aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kudhibiti viwanda vinavyomwaga maji machafu kwenye mito wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam.

Mhe. Kwagilwa alisema kuwa Serikali kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti viwanda vinavyomwaga maji machafu kwenye mito.

Alitaja hatua hizo kuwa ni kufanya kaguzi za mara kwa mara katika viwanda vilivyopo Temeke, kupima ubora wa majitaka yanayotiririshwa kwenye mito na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya viwanda vinavyokiuka Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191 pamoja na Sheria ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, Sura ya 272.

Mhe. Kwagilwa aliongeza kuwa katika kudhibiti changamoto ya viwanda kutiririsha maji machafu kwenye mito, Serikali inatoa maagizo ya kurekebisha au kusimamisha shughuli za viwanda vinavyosababisha uchafuzi wa mazingira.

Naibu Waziri huyo alieleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha doria za mazingira, kufanya kaguzi za kushtukiza na kutoa elimu kwa wamiliki wa viwanda vilivyopo Temeke na maeneo mengine nchini.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kwagilwa aliwaelekeza mameneja wa kanda zote za NEMC wasimamie utekelezaji wa sheria ya mazingira na usafi wa mazingira ili kuhakikisha uzalishaji wa bidhaa viwandani na madini migodini hauathiri mazingira.

Alitoa maelekezo hayo wakati akijibu maswali ya nyongeza kutoka kwa Mhe. Kisangi na Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Lucy Kombani kuhusu Serikali imechukua hatua gani kwa wanaochafua mazingira kupitia migodi.