MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSF), Fortunatus Magambo, ameendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu baada ya kujitolea kujenga vyumba vitano vya madarasa katika Shule ya Msingi Ring’wani iliyopo Kata ya Nyamatare.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya mshikamano wa wadau wa maendeleo katika kuunga mkono dhamira ya Rais Samia ya kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia nchini kote kupitia uboreshaji wa miundombinu ya elimu.
Akizungumza kuhusu uamuzi wake huo, Bw. Magambo amesema aliguswa na hali halisi ya shule hiyo baada ya kuitembelea mwaka 2024 na kushuhudia changamoto kubwa ya upungufu wa madarasa pamoja na uchakavu wa baadhi ya miundombinu iliyokuwa ikiathiri mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
“Nilipofika hapa niliona namna watoto wanavyopata shida kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa. Hivyo nimeona ni vyema nami kushiriki kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya elimu ili watoto wetu wapate mazingira mazuri ya kusoma,” amesema Magambo.
Kwa mujibu wa taarifa za mradi huo, tayari kazi za awali za ujenzi ikiwemo uchimbaji wa msingi zimeanza huku matarajio yakiwa ni kukamilika kwa vyumba hivyo kabla ya Julai mwaka 2026 kuisha.
Diwani wa Kata ya Nyamatare, Mgaya Maheke, amesema hatua ya Magambo ni mfano mzuri wa namna wadau binafsi wanavyoweza kushirikiana na serikali katika kuharakisha maendeleo ya jamii, hususan katika sekta ya elimu ambayo ni msingi wa maendeleo ya taifa.
“Tunamshukuru sana Bw. Magambo kwa moyo wake wa kujitoa kusaidia wananchi wetu. Hii ni ishara nzuri ya kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Samia katika kuboresha elimu nchini,” amesema Maheke.
Aidha, amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali, wadau wa maendeleo na wananchi ni muhimu katika kuhakikisha changamoto mbalimbali za kijamii zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu kupitia ujenzi wa shule mpya, vyumba vya madarasa, mabweni, maabara pamoja na miundombinu mingine muhimu ya kujifunzia na kufundishia.
Kutokana na juhudi hizo, wadau mbalimbali wameendelea kujitokeza kushiriki katika kuimarisha sekta hiyo kwa kutambua kuwa elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

