RPC MORCASE: PWANI SI NJIA YA MKATO, WATAKAMATWA
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mei 10, 2026
JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limetoa onyo kali kwa wanaojihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya, ikiwemo mirungi na bangi, kupitia barabara za mkoa huo, likisisitiza kuwa hakuna njia za mkato kwani wataendelea kukamatwa .
Katika kuhakikisha linadhibiti vitendo hivyo, jeshi hilo limekamata magari mawili ,zaidi ya kilogramu 800 za mirungi pamoja na kilogramu 62.7 za bangi kupitia misako na operesheni zilizofanyika katika kipindi cha miezi miwili kuanzia Machi hadi Aprili 2026.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, alisema katika eneo la Dagaza, Zinga wilayani Bagamoyo, polisi walikamata gari aina ya Alphard lenye namba T 889 DYZ likiwa na mifuko tisa ya sandarusi yenye mabunda 419 ya mirungi sawa na kilogramu 315.
Aidha, katika kizuizi cha Maliasili Msata, Chalinze, polisi waliwakamata wakazi wawili wa Korogwe mkoani Tanga wakiwa ndani ya gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 lenye namba T 422 CNS wakisafirisha mabunda 548 ya mirungi yenye uzito wa kilogramu 387.3 kutoka Kilimanjaro kuelekea Dar es Salaam.
Vilevile Morcase alieleza ,wamekamata kilogramu 98.3 za mirungi katika matukio mengine pamoja na kilogramu 62.7 za bangi.
Alisema usafirishaji wa mirungi na bangi umeendelea kushika kasi, hali inayosababisha jeshi hilo kuongeza nguvu katika operesheni za kuwabaini na kuwakamata wahusika.
“Mkoa wa Pwani upo salama, Sio mara ya kwanza wahalifu hawa kutumia barabara za Pwani wakiamini Dar es Salaam kuna soko la dawa hizo, ;Wajitathmini, kwa sababu hakuna njia ya mkato; iwe barabarani ama ardhini watakamatwa ,” alibainisha Morcase.
Kutokana na misako hiyo, jumla ya watu 261 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali ya kiuhalifu, silaha tano zilizokuwa zikitumika kinyume cha sheria, nyara za serikali, lita 220 za mafuta ya dizeli, runinga nane, magari matano, simu za mkononi, sabufa na pikipiki.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limetangaza vita dhidi ya vitendo vya ubakaji, ulawiti na unyanyasaji wa kijinsia, huku likieleza yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kifungo cha jela.
