Mbunge aomba barabara ya lami, Halmashauri ya Kibakwe
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amerejesha furaha kwa Bi. Federica Masangasi wa kijiji cha Muungano wilayani Mpwapwa kwa kumpatia godoro na kitanda.
Bi. Federica alijitokeza kwenye mkutano wa hadhara na kuandika kero yake ya kutekelezwa na mumewe, Bw. Erenei Ngilikule tangu mwaka 2011 na kumuachia watoto sita.
Akielezea kero hiyo, Bi. Federica alisema mumewe ambaye ni mwalimu, alimtelekeza bila matunzo ya watoto na hata alipofikishwa kwa mtendaji hakutekeleza maagizo aliyopewa. Aliomba apewe kitanda na godoro kwa sababu yeye na wanaye wanalala kwenye salfeti.
Waziri Mkuu amefikia uamuzi huo leo (Jumamosi, Mei 9, 2026) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano uliofanyika stendi ya Kibakwe, wilayani Mpwapwa, mkoani Dodoma. Akiwa hapo alisikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alimwelekeza Afisa Tarafa ya Kibakwe, Bw. Nusuru Tegete amjulishe muwe wa Federica kwamba anapewa onyo la mwisho kuhusu kutoa matunzo kwa familia yake na asipotekeleza, atashtakiwa kwa mwajiri wake.
“Binafsi ninakupongeza Bw. Tegete kwa kufuatilia suala la huyu Mama wakati ukiwa Mtendaji wa Kata na kuamua kumuita mhusika. Kitendo ulichofanya, ndicho Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona kinafanyika, kitendo cha kuleta tabasamu kwa Watanzania,” amesema.
Kabla ya kuzungumza na wakazi hao, Dkt. Mwigulu alipokea taarifa ya mradi wa soko la mazao Kibakwe litakaloweza kuchukua wafanyabiashara 350 na kisha akaweka jiwe la msingi na kufungua soko hilo.
Akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Athumani Kilundumya alisema soko hilo ni miongoni mwa masoko mengine manne yanayoendelea kujengwa katika Wilaya za Karatu, Monduli na Nzega kwa gharama ya sh. bilioni 3.4 ambayo kwa ujumla ujenzi wake umefikia asilimia 64.
Alisema kwa soko la Kibakwe pekee, ujenzi wake umefikia asilimia 98 na kazi zilizobakia kwa sasa ni ndogondogo za kumalizia.
Mapema, Mbunge wa jimbo la Kibakwe, George Simbachawene alimuomba Waziri Mkuu awasaidie kutafuta fedha za ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kibakwe hadi Mpwapwa yalipo makao makuu ya wilaya ya Mpwapwa.
“Hii wilaya ni kongwe. Ni miongoni mwa wilaya tisa za mwanzo wakati nchi yetu inapata uhuru lakini haina barabara za lami. Tunaomba fedha ipatikane ili mkandarasi atafutwe na hatimaye barabara ijengwe,” alisema.
Pia aliomba iundwe Halmashauri ya Kibakwe ili iwe rahisi kusogeza huduma muhimu kwa wananchi walioko maeneo ya milimani. “Jimbo la Kibakwe lina kata 18 lakini kata nane kati ya hizo, zina jiografia ngumu. Kata hizi ziko milimani na zina ugumu wa kufikika,” alisema.
Aliishukuru serikali kwa kupeleka fedha za miradi mbalimbali kwenye sekta za afya, elimu, na maji. Pia, alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutenga muda na kufanya ziara wilayani Mpwapwa miezi michache baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
