*Asema Pori la akiba Mpanga Kipengere ni moja ya kivutio kinachopaswa kutangazwa duniani.
*Aipongeza Wizara ya Maliasili kwa Uhifadhi na kuhamasisha Utalii
Na Neema Chalila Mbuja, Njombe
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, utamaduni, sanaa na michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bwana Gerson Msigwa,amewataka maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini kutangaza vivutio vipya vya utalii vilivyoko hapa nchini ili kuonesha na kutoa fursa ya kujulikana nchini na duniani kwa ujumla.
Msigwa ameyasema hayo wakati wa ziara ya maafisa Habari Uhusiano na Itifaki walipotembelea hifadhi ya Pori la Akiba la Mpanga Kipengere ikiwa ni mwendelezo wa kikao kazi cha 21 ya Maafisa habari kinachoendelea mkoani Njombe.
Amesema Maafisa Habari wanayo nafasi kubwa ya kuonesha na kuieleza dunia juu ya utajiri wa Maliasili iliyopo Tanzania na kuitangaza hususani katika kipindi cha kuelekea katika michuano ya Mpira wa miguu ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON -2027) ambapo Tanzania itapokea Wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali Afrika na duniani kwa ujumla.
‘’ Dhamira ya Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na utalii ni kufungua fursa na kuhakikisha utalii unakua kwa Kiasi kikubwa Kama moja ya sekta zenye uchochezi mkubwa kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050’’ Alisisitiza Bwana Msigwa.
Kwa upande wao baadhi ya maafisa habari waliohojiwa mara baada ya kutembelea kivutio hicho Bi Rhoida Andusamile kutoka TAMISEMI amesema,kila Afisa Mawasiliano anajukumu la kutangaza utalii kwakuwa faida inayotokana na Utalii ni kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.
Naye Bi Zawadi Msala na Bwana Eliezer Rwekiza kutoka AICC wamesema kufanyika kwa mashindano ya AFCON hapa nchini ni fursa inayopaswa kutumiwa vyema na Maafisa Habari wote wa Serikali ili kutangaza utalii wa mazingira, matibabu , na mikutano ya kimataifa kwani ni sehemu ya utalii
Wameongeza kuwa eneo la hifadhi ya pori la akiba la Mpanga kipengere ni moja ya kivutio kikubwa kwa utalii na kuitaka Wizara ya maliasili na utalii kufungua fursa zaidi za uwekezaji kwenye eneo hilo lenye historia kubwa kwenye nchi yetu.
Hifadhi ya pori la akiba la Mpanga kipengere lina ukubwa wa mita za mraba 1574 na maporomoko yake ya maji kwenye eneo hilo ni takribani mita 700 na linasimiwa na na mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori-TAWA na lina mwinuko wa takribani mita 1,300 hadi 3,000 kutoka Sawa wa bahari

