Mkurugenzi wa Halmashauri Arusha , Suleiman Msumi akizungumza kwenye baraza hilo jijini Arusha
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha DC, Baraka Mesiaki akizungumza kwenye baraza hilo.
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Mkurugenzi wa Halmashauri Arusha , Suleiman Msumi amesema kuwa,wameanza kufanya matengenezo ya barabara ya Korofi eneo la Sekei ikiwa ni maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Ahmed Mwinyi.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Arusha DC, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Suleiman Msumi, amesema tayari kazi za matengenezo zimeanza ambapo greda limeanza kusawazisha barabara sambamba na uwekaji wa zaidi ya tani 150 za vifusi.
“maboresho hayo yataanzia eneo la Sekei hadi mwisho wa Shule ya Ngeresi kwa lengo la kuhakikisha barabara hiyo inapitika kwa urahisi katika kipindi chote cha mwaka.”amesema Msumi.
Aidha, amesema barabara hiyo tayari imeingizwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami ambapo kwa sasa, juhudi zinaelekezwa katika uwekaji wa vifusi pamoja na kuboresha mifumo ya kupitisha maji ili kupunguza athari za mvua zinazoendelea kunyesha ambapo amesema kazi hiyo inafanywa na TARURA.
Aidha Msumi amewataka madiwani kuwa na subira huku akieleza kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Ahmed Mwinyi, yuko Dodoma kwa mazungumzo na Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, ili kuomba fedha za dharura kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara katika Halmashauri ya Arusha DC.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha DC, Baraka Mesiaki amesema zaidi ya shilingi bilioni 2 zimetengwa na TARURA kwa ajili ya kuboresha barabara katika kata zote 27 za halmashauri hiyo, baada ya nyingi kuharibika kutokana na mvua kubwa.

