Na Saidi Saidi, WMJJWM – Dodoma

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka madiwani na viongozi wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi mkoani Dodoma kuhakikisha agenda ya uwezeshaji wanawake kiuchumi inatekelezwa kwa vitendo kupitia mipango na bajeti za maendeleo katika halmashauri zao.

Dkt. Gwajima amesema hayo leo Mei 8, 2026, jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha madiwani pamoja na viongozi wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi. Amesema majukwaa hayo ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, yenye lengo la kuwainua wanawake kiuchumi kupitia elimu ya fedha, ujasiriamali, matumizi ya teknolojia pamoja na upatikanaji wa mikopo na masoko.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanawake wanapata taarifa sahihi, wanaunganishwa katika vikundi na kushiriki kikamilifu katika majukwaa hayo ili wasiachewe nyuma kutokana na ukosefu wa taarifa au usimamizi hafifu. Pia amewataka madiwani kushirikiana na taasisi za fedha, sekta binafsi pamoja na wataalam ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanawake.

Dkt. Gwajima ameongeza kuwa Tanzania inaweza kufikia uchumi jumuishi na malengo ya Dira ya Taifa ya 2050 endapo kutakuwa na ushirikiano, uwajibikaji na dhamira ya kweli ya kumuinua mwanamke kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka wizara hiyo, Badru Abdunur, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara, amewasisitiza washiriki kuzingatia mafunzo ya Mwongozo wa Uundaji na Uratibu wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa wenye tija.

Naye Joan Mazanda, akizungumza kwa niaba ya madiwani na viongozi wa majukwaa hayo, amesema wako tayari kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Waziri Dkt. Gwajima ili kuhakikisha wanawake wanapata fursa za kiuchumi kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.