Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma 

Serikali kupitia Wizara ya Maji imeendelea na maandalizi ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa Bwawa la Farkwa utakaogharimu Shilingi bilioni 312 kwa lengo la kuimarisha huduma ya maji katika Jiji la Dodoma na maeneo ya jirani.

Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa muda wa kati wa Serikali wa kuhakikisha upatikanaji wa maji wa uhakika katika makao makuu ya nchi.

Amesema kuwa bwawa hilo litanufaisha wakazi wa Jiji la Dodoma pamoja na Wilaya za Chemba, Bahi na Chamwino ambazo zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kutokana na hali ya ukame.

“Mradi huo unahusisha ujenzi wa bwawa pamoja na mtambo wa kusafisha na kutibu maji wenye uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 128,000 za maji kwa siku,” amesema Aweso

Waziri Aweso amesema kuwa tayari mkandarasi wa ujenzi amepatikana na hatua za kusaini mkataba zinaendelea kabla ya kuanza rasmi kwa kazi za ujenzi.

Amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aweso ameongeza kuwa uwekezaji huo utaimarisha shughuli za kijamii na kiuchumi katika Jiji la Dodoma ambalo linaendelea kukua kwa kasi kutokana na kuhamia kwa shughuli nyingi za Serikali.