Dar es Salaam, Mei 5, 2026

Chama cha Wafanyakazi wa Wakusanya Mapato Tanzania (TAREWU) kimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) na Taasisi ya Usimamizi wa Vihatarishi Tanzania (IRMT) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika maendeleo ya kitaaluma na mafunzo ya usimamizi wa vihatarishi.

Makubaliano hayo yamesainiwa jijini Dar es Salaam, yakilenga kuwajengea uwezo wanachama wa TAREWU ili kuongeza ufanisi na tija katika sekta ya ukusanyaji mapato nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa IRMT, CPA Pius Maneno, amesema taasisi yake ipo tayari kutoa mafunzo yenye viwango vya kimataifa na kushirikiana katika kukuza taaluma ya usimamizi wa vihatarishi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAREWU, Lutufyo Mtafya, amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mpango mkakati wa chama hicho unaolenga kuwafanya wanachama wake kuwa na ujuzi shindani unaoendana na mabadiliko ya kiuchumi duniani.

Amesema kupitia ushirikiano huo, wanachama watanufaika na programu za mafunzo, ushauri wa kitaalamu pamoja na fursa za kukuza ujuzi katika maeneo ya kisasa ya usimamizi wa vihatarishi.

Naye Katibu wa IRMT, Christopher Njovu, amesema ushirikiano huo utasaidia kuongeza uelewa wa masuala ya vihatarishi katika sekta ya ukusanyaji mapato na kusisitiza umuhimu wa taaluma hiyo katika kulinda rasilimali za taasisi.

Kwa upande wa TAREWU, Katibu wake, Wakili Michael Marere, amesema makubaliano hayo yatakuwa chachu ya maendeleo endelevu kwa wanachama na sekta nzima ya mapato nchini.

TAREWU imeeleza kuwa ina imani ushirikiano huo utafungua ukurasa mpya wa mafanikio, huku IRMT ikiahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.