MFANYABIASHARA wa vifaa vya umeme kutoka mkoa wa Njombe, Erick Sambala, ameomba msaada wa spika kupatiwa haki yake baada ya kudaiwa kukwama kibiashara kutokana na deni ambalo anamdai mbunge wa viti maalum Siglada Mligo.Akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa, Sambala anadai alifanya biashara ya vifaa vya muziki na mbunge huyo yenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 18.5 makubaliano kuwa malipo yangekamilishwa ndani ya miezi mitatu. Hata hivyo, ni shilingi milioni 8.5 pekee ndizo alizolipwa, huku kiasi kilichobaki cha shilingi milioni 11 baada hukumu kikiwa hakijalipwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili sasa.
Kwa mujibu wa maelezo yake, baada ya kuona malipo hayatolewi kama walivyokubaliana, alichukua hatua za kisheria kwa kufungua kesi katika Mahakama ya Mwanzo mjini Njombe ambako aliibuka mshindi.
Sambala alisema kuwa Baada ya hapo, upande wa mbunge ulikata rufaa katika Mahakama ya Wilaya, lakini mfanyabiashara huyo aliendelea kushinda hata katika ngazi hiyo ya juu zaidi.
Pamoja na uamuzi wa mahakama kuwa upande wake, Sambala anadai mbunge huyo ameendelea kukataa kutekeleza hukumu na amelalamika kuwa kitendo hicho kimemrudisha nyuma kimaendeleo.
Ameeleza kuwa biashara yake imedorora, ameshindwa kugharamia elimu ya watoto wake na kuona maisha yakizidi kuwa magumu kutokana na kukosa mtaji wake halisi.
Amesema ni jambo la kusikitisha kuona mtu anayehusika kutetea haki za wananchi ndiye anayeshindwa kuheshimu haki ya mwananchi wa kawaida, huku akisisitiza kuwa hana uwezo wa kuendelea na shughuli zake za kimaendeleo mpaka atakapopata fedha zake zilizobaki.
Sambala amemuomba Spika wa Bunge Idd Hassan Zungu kuingilia kati, ili kuhakikisha anapatiwa haki yake na kurejeshewa fedha zake ili aweze kuendeleza shughuli zake za kibiashara.
Aliongeza kuwa baada ya kuona hakuna utekelezaji wa makubaliano yao Sambala ameamua kupaza sauti kupitia vyombo vya habari ili aweze kupatiwa haki yake.
“Pamoja na maamuzi hayo mawili ya mahakama, Sambala anadai kuwa mbunge huyo ameshindwa kutekeleza hukumu na kuendelea kutoa ahadi ambazo hazijatimia hadi sasa kwani kwa miaka miwili sasa nimehangaika kupata haki yangu licha ya Mahakama kunipa ushindi mara mbili, lakini bado sijalipwa” alisema
Sambala alisema kuwa kutokana na hali hiyo ametumia gharama kubwa katika kuendesha kesi hizo kwa kuwalipa mawakili na gharama nyingine kama usafiri ambazo anasema atazidai katika Mahakama alipwe.
Kama full shangwe hatukuishia kuandika habari ya chanzo kimoja saa kumi na dk 56 tuliweza mpigia simu Mbunge Siglada Mligo kwa namba yake inayoishia ….579 na mahojiano kati ya mwandishi na mhusika yalikuwa kama hivii
Mwandishi:
Habari za leo Mh.Siglada salama?
Mhusika:
Salama.
Mwandishi:
Naitwa Dennis Mlowe, mwandishi wa habari kutoka Iringa mjini.
Mhusika:
Dennis nani?
Mwandishi:
Dennis Mlowe.
Mhusika:
Sawa, endelea.
Mwandishi:
Kuna taarifa tumepokea kupitia kwa mtu anayeitwa Eric Sambala. Ameibua madai kuwa unadaiwa kiasi cha fedha ambacho kilitakiwa kulipwa lakini hadi sasa, kwa mujibu wake, haujalipa. Lengo langu kukupigia ni kupata upande wako wa maelezo kuhusu madai haya. Unaweza kufafanua?
Mhusika:
Wewe ni mwandishi wa habari?
Mwandishi:
Ndio, ni mwandishi wa habari.
Mhusika:
Na uliona wapi suala hilo?
Mwandishi:
Amefika ofisini kwa wandishi wa habari mkoa wa Iringa na kutoa malalamiko haya hadharani.
Mhusika:
Lakini hiyo si kazi yenu?
Mwandishi:
Ndiyo, ametoa taarifa mbele ya waandishi wa habari sisi waandishi ndiyo tuliopewa taarifa.
Mhusika:
Hiyo si kazi yenu?
Mwandishi:
Ni waandishi wa habari. Ametuletea taarifa.
Mhusika:
Hiyo si kazi yenu?
Mwandishi:
(Anajaribu kufafanua zaidi) Ni utaratibu wa kawaida mtu kutoa taarifa kwa waandishi wa habari. Ndicho alichokifanya mhusika
Mhusika:
Hiyo si kazi yenu?
Mwandishi:
(Anarejea swali) Taarifa ametoa kwa waandishi wa habari sisi ili tupate upande wako pia.
Mhusika
Andikeni ….titititititti
Simu imekatwa….
Hivyo ndio hali halisi kati ya mwandishi wa habari hizi na mbunge Siglada Mligo ambaye hukutaka kuongea zaidi.

