Na Maelezo Zanzibar 

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini Joseph John Kilangi amesema waandishi wa habari wana jukumu la kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kulinda afya na mazingira.

Akifungua warsha ya uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi kwa waandishi wa habari iliyofanyika katika Hotel Verde Mtoni, amesema Zanzibar imekuwa inakumbana na changamoto katika kubadilisha mitazamo ya wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Ameeleza kuwa matumizi ya nishati safi kama gesi na umeme husaidia kupunguza maradhi yanayosababishwa na moshi, ikiwemo pumu na kifua kikuu (TB), yanayotokana na  matumizi ya nishati asili ya kuni na makaa.

“Jamii inapaswa kutumia nishati safi kwa matumizi ya kupikia ikiwemo gesi na umeme ili kujiepusha na maradhi yanayoweza kuepukika yakiwemo pumu na kifua kikuu (TB)” ameeleza Kilangi.

Hata hivyo amefahamisha kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha wananchi juu ya matumizi sahihi ya nishati safi nchini ikiwemo nishati ya kupikia.

Amefahamisha kuwa mashirika mbali mbali yamekuwa yakiunga mkono jitihada za Serikali katika kuhamasisha jamii juu ya matumizi ya nishati safi ili kuzuia uharibifu wa mazingira.

Aidha amewataka waandishi wa habari kuandaa na kuanzisha vipindi na makala zenye maudhui ya kuhamasisha jamii kuhusu faida za matumizi sahihi ya nishati safi.

Hata hivyo amesisitiza  jamii kupunguza ukataji miti na kuhimiza upandaji miti kwa kulinda mazingira na mabadiliko ya tabianchi ili kuhakikisha vizazi vijavyo vinaishi katika mazingira salama.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Nishati Sayyedomar Abdalla Idarous, amesema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 58 ya wananchi hutumia kuni na asilimia 56 hutumia makaa hali inayochangia kwa kiasi kikubwa athari za kiafya na kimazingira.

Warsha hiyo ya Siku mbili ya Mradi wa pamoja wa Zanzibar imeandaliwa na Shirika la Kimataifa la Mitaji ya Maendeleo UNCDF kwa kushirikiana Serikali ya Norway.