Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limemkamata mmiliki wa eneo linalohusishwa na mgogoro wa ardhi uliosababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi wengine 14 katika eneo la Vikawe (Lupaso), Kata ya Pangani, Wilaya ya Kibaha mkoani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Mei 6, 2026, baada ya watu wanaodaiwa kutumwa kufika eneo hilo na kufanya ubomoaji wa nyumba pamoja na kushambulia baadhi ya wananchi.

Akizungumzia tukio hilo baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa kuzungumzia kadhia hiyo siku ya tukio, Morcase alieleza Ofisi ya Upelelezi Mkoa inaendelea kumhoji mtuhumiwa kuhusiana na tukio hilo lililosababisha madhara makubwa .

Alisema jina la mtuhumiwa huyo linahifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Morcase alibainisha kuwa baadhi ya majeruhi 14 wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi, huku majeruhi mmoja amehamishiwa Hospitali ya Mloganzila (Muhas) kwa matibabu zaidi kutokana na majeraha aliyoyapata.

Kamanda huyo alielezea idadi ya vifo haijaongezeka, huku majina ya marehemu yakiwa bado hayajafahamika ambapo amewaomba wakazi wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani ambao hawajawaona ndugu zao kufika Hospitali ya Tumbi kwa ajili ya utambuzi.

Katika tukio hilo Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, aliwataka wananchi kujiepusha kujichukulia sheria mkononi na kuvamia maeneo yasiyo yao.

Kadhalika, aliwaasa wamiliki wa ardhi kuwa endapo kuna amri ya mahakama ya kubomoa nyumba, washirikishe vyombo vya dola badala ya kuchukua hatua binafsi.

Nyumba zaidi ya 10 zimedaiwa kubomolewa, kati ya hizo nyumba saba pamoja na maboma, huku baadhi ya wananchi wakidai kushambuliwa, kuibiwa vitu mbalimbali, simu na fedha wakati wa vurugu hizo.