Na John Bukuku
Mwenyekiti wa Chama cha Wazee Wanaume Tanzania, Bw. Tadey Mchena, amelaani vikali kitendo kinachodaiwa kufanywa na mzee mmoja anayejulikana kwa jina la Malundo, akisema hakikubaliki katika jamii na kinakiuka maadili pamoja na haki za binadamu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mchena ambaye pia ni Rais wa chama hicho, amesema kumekuwa na video inayosambaa katika mitandao ya kijamii ikimuonesha mzee huyo akijisifia kuwa amekuwa na mahusiano na wanawake 131, jambo alilosema linakwenda kinyume na maadili ya Kitanzania.
Amesisitiza kuwa kitendo hicho ni cha ovyo na hakipaswi kuvumiliwa, hasa kwa kuzingatia umri wa mhusika, akieleza kuwa wazee wanapaswa kuwa mfano bora kwa jamii badala ya kuhamasisha mienendo isiyofaa.
“Kwa kweli kitendo hiki hakikubaliki kabisa katika jamii yetu. Mzee wa umri huo anatakiwa kufundisha maadili mema, lakini badala yake anajisifia mambo ambayo hayana maadili,” amesema Mchena.
Aidha, ameomba Serikali na mamlaka husika kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mhusika huyo ili kutoa funzo kwa jamii na kuzuia matukio kama hayo kujirudia.
Mchena ameongeza kuwa kitendo hicho kimempa wasiwasi mkubwa, akieleza kuwa si kawaida kwa mtu mwenye umri mkubwa na akili timamu kufanya vitendo vya namna hiyo na kuvieneza hadharani.
Kwa upande mwingine, ametoa wito kwa Watanzania kujiunga na chama hicho ili kusaidia kurejesha maadili katika jamii, hasa kwa vijana ambao wamekuwa wakikumbwa na mmomonyoko wa maadili.
“Niwaombe Watanzania wote wenye umri kuanzia miaka 50 wajiunge na Chama cha Wazee Wanaume Tanzania ili kwa pamoja tuisaidie Serikali kurejesha maadili yaliyopotea,” amesisitiza.
Chama cha Wazee Wanaume Tanzania kina makao yake makuu katika Arusha, kikiwa na kaulimbiu isemayo “Wazee ni tunu, tuwalinde.”
Aidha, chama hicho kinatarajia kufanya mkutano wake mkuu Juni 13, 2026 katika Dodoma, ambapo masuala mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa wazee yatajadiliwa.
