Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA imesaini makubaliano na kampuni ya mtandao wa simu wa AitelTanzania kwa lengo la kuimarisha mafunzo ya ufundi satdi kwa njia za kidigiatali (VSOMO APP), Programu hii itawawezesha vijana kujifunza kozi mbalimbali popote walipo na watakapohitimu watatunukiwa vyeti vya VETA.
Makubaliano hayo yamesaini tarehe 5 Mei, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya simu Airtel Tanzania Bw. Charles Kamoto kwenye ofisi za Airtel Tanzania Kinondoni jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa hati ya makubaliano yaliyosainiwa, makubaliano hayo yanalenga kuleta mabadiliko chanya katika utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa njia za kidigitali kwani kupitia VSOMO APP mtu atapata mafunzo ya nadharia (theory) moja kwa moja kupitia simu yake ya mkononi, hivyo hatahitaji kuwa darasani muda wote.
Sambamba na hilo Baada ya kumaliza masomo ya nadharia kwenye simu, mwanafunzi anaweza kwenda katika chuo chochote cha VETA kilicho karibu nayeye ili kukamilisha mafunzo ya vitendo.
Aidha kupitia VSOMO APP mwanafuzi ataweza kujifunza masomo ya ufundi kwa lugha ya Kiswahili na Kingereza, jambo ambalo litafanya uelewa kuwa rahisi kwa kila mtumiaji na baada ya kumaliza mafunzo mwanafunzi atapatiwa cheti cha VETA, ambacho kitamuweza kupata ajira au kujiajiri mwenyewe.
Akizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore amesema VSOMO APP ni jukwaa kubwa linalo waweza wananchi kupata mafunzo kwa njia ya kidigitali kupitia teknolojia ya simu,kompyuta na vishikwambi.
“kwa upande wetu sisi kama VETA tumekuwa tukiutumia mfumo huu,kulingana na jukumu tulilonalo lakutoa mafunzo mfumo huu unatusaidia kuwafikia watanzania popote walipo kwa urahisi” amebainisha Kasore.
CPA Kasore ameongeza kuwa jukwaa la VSOMO APP pia limeunganishwa na mfumo wa Fundi Connect, unaowawezesha wahitimu wa VETA kusajili ujuzi wao na kuunganishwa moja kwa moja na wateja, hivyo kuimarisha uhusiano kati ya mafunzo na ajira pamoja na kusaidia ujasiriamali wa vijana.
Sambamba na hilo Kasore amesema ushirikiano huo unaunga mkono ajenda ya maendeleo ya taifa chini ya Dira ya Maendeleo 2030, na kuimarisha juhudi za serikali za kuongeza ajira kwa vijana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Tunaishukuru sana Airtel Tanzania kwa msaada wao endelevu, hasa katika kutoa huduma ya intaneti na kuwezesha upatikanaji mpana wa VSOMO. Ushirikiano huu umetuwezesha kuwafikia vijana wengi zaidi kuliko hapo awali lakini pia tunashukuru serikali ya awamu ya sita na wizara ya Elimu kwa kuendelea kuwekeza katika Elimu ya Ufundi ,” alisema Kasore
Kasore amebainisha kuwa kupitia VSOMO, VETA imelenga la kuwafikia wanafunzi 400 wapya kila mwezi, kama sehemu ya kuendelea kupanua elimu ya ujuzi wa kidigitali na kuimarisha ajira kwa vijana nchini
“Kupitia VSOMO, tunapanua wigo ili vijana wengi zaidi wapate ujuzi wa vitendo kwa ajili ya ajira na kujiajiri popote walipo,” alisema.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya Airtel katika kuendeleza mageuzi jumuishi ya kidigitali na kupanua upatikanaji wa elimu ya ujuzi kwa Watanzania.
“Airtel VSOMO ni jukwaa rasmi la taifa la mafunzo ya ufundi stadi mtandaoni chini ya VETA. Linawawezesha Watanzania kupata ujuzi wa vitendo wakati wowote na mahali popote kupitia vifaa vyao vya kidigitali,” alisema Kamoto.
Aidha Kamoto alisisitiza kuwa mchango wa Airtel hauishii kwenye mawasiliano pekee, bali unajumuisha uwekezaji mpana katika ujumuishaji wa kidigitali, elimu na uwezeshaji wa vijana.
“Sisi Airtel hatujihusishi tu na kutoa huduma ya mtandao. Tunahamasisha kikamilifu matumizi ya Airtel VSOMO, tunatoa huduma ya bila gharama ya data, na kuhakikisha gharama si kikwazo kwa Watanzania kujifunza na kujiendeleza,” aliongeza
Kwa upande wake Beatrice Singano Mkurugenzi wa mawasiliano toka Kampuni ya Airtel Tanzania amesema VSOMO inasiadia vijana wengi kusoma kupitia mtandao huku wakiendelea na shughuli zao nyinge za uzalishaji.
“tuliwauliza vijana wengi wakasema kozi za VETA zina maufaa makubwa kwao lakini hawana muda wakwenda kukaa darasani muda mrefu,hivyo kwa kupitia VSOMO vija watatumia muda mchache kusoma kupiti simu zao huku wakiendelea na shughuli zao za uzalishaji bila kuathirika” alisema Beatrice.
Takwimu za Airtel zinaonesha kuwa Airtel VSOMO imepakuliwa mara 59,000, ambapo takribani asilimia 60 ya matumizi yamefanyika kupitia huduma ya bure ya data ya Airtel. Jumla ya watumiaji 27,194 wamejisajili kwenye jukwaa hilo, huku wanafunzi 9,539 wakijiunga na programu mbalimbali za ufundi stadi.
Kati ya hao, wanafunzi 6,723 tayari wamehitimu mafunzo yao, jambo linaloonesha ongezeko la matumizi na mafanikio katika elimu ya ufundi stadi ya kidigitali.

