NA DENIS MLOWE, IRINGA
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Iringa limekaa chini katika kikao na kujadili kwa kina changamoto mbalimbali zinazoikabili wananchi, huku hoja nyingi zikijikita katika ubovu wa miundombinu ya barabara, ucheleweshaji wa ujenzi wa vibanda vya wafanyabiashara na ongezeko la shughuli za ujasiriamali zinazoathiri matumizi sahihi ya maeneo ya barabarani.
Madiwani hao wameitaka halmashauri kuongeza kasi ya ufuatiliaji, usimamizi na mawasiliano na taasisi zinazohusika ili kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Katika kikao hicho, baadhi ya madiwani walielezea hali mbaya ya baadhi ya barabara ndani ya manispaa, wakisema kuwa hazipitiki kwa usalama kutokana na mashimo na uharibifu uliokithiri.
Walitaja kuwa pamoja na changamoto za bajeti, kuna haja ya dharura ya kushirikiana kwa karibu na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) ili kuhakikisha maeneo yaliyoharibika yanafanyiwa matengenezo ya haraka.
Madiwani walisisitiza kuwa barabara zinazohudumiwa na taasisi hiyo zinahitaji ufuatiliaji wa kitaalamu, na ofisi ya mhandisi wa manispaa inapaswa kuhakikisha taarifa za kina zinawasilishwa na kushughulikiwa kwa wakati.
Aidha, ilielezwa kuwa baadhi ya maeneo yanayopitiwa na wanafunzi na wafanyakazi wa vyuo, pamoja na wakazi wa kawaida, yamekuwa kero kutokana na uharibifu wa barabara unaoendelea kukua. Madiwani walisema kuwa barabara hizo ni muhimu katika kuunganisha watu kutoka kata moja hadi nyingine, hivyo kuchelewa kwa matengenezo kunahatarisha usalama wa watumiaji na kuathiri shughuli za kiuchumi.
Katika hoja nyingine, kikao kilipokea taarifa kuhusu ujenzi wa vibanda katika eneo la Masai Market lililoko bustani ya posta ambalo awali liliungua moto na Ilielezwa kuwa ujenzi huo sasa unaendelea, na wadau waliojitokeza kusaidia wanahakikisha mradi huo unakamilika kama ilivyopangwa.
Hata hivyo, kabla ya kuanza ujenzi, halmashauri ililazimika kusitisha kutoa kibali cha machinga kurudi katika eneo hilo kwa muda kutokana na hofu ya uwezekano wa moto kujirudia. Ilielezwa kuwa vifaa vilivyokuwa vinatumiwa awali, ambavyo vilijengwa kwa mbao, vingeweza kuongeza hatari kama moto ungekuwa bado haujadhibitiwa kikamilifu.
Uongozi wa manispaa ulifafanua kuwa licha ya machinga kuhitaji kurejea kwenye vibanda vyao mapema, kulikuwa na ulazima wa kuhakikisha eneo hilo linafanyiwa tathmini ya usalama kwanza. Zaidi ya hapo, baadhi ya wafanyabiashara walionekana kuwa na uwezo mdogo wa kuendelea na ujenzi bila msaada, hivyo halmashauri iliendelea kuwasiliana na wadau hadi mmoja wao alipojitokeza kusaidia ujenzi kwa kiwango kikubwa.
Katika hatua nyingine ya mjadala, Diwani Godfrey Mlowe alitoa hoja kuhusu changamoto za shughuli za ujasiriamali zinazofanyika karibu na barabara zinazoelekea kwenye vibanda vya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema kuwa eneo hilo limekuwa likikumbana na msongamano wa shughuli kama gereji za kutengeneza pikipiki ambazo kwa sasa zimeenea hadi ndani ya barabara.
Aliongeza kuwa vijana wanaofanya shughuli hizo ni muhimu katika uchumi wa manispaa, lakini ni lazima kuandaliwa maeneo maalumu ili waweze kufanya kazi zao bila kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Diwani huyo alikumbusha kuwa halmashauri imekuwa ikijadili kwa muda mrefu suala la kuhamisha shughuli hizo kutoka barabarani, lakini utekelezaji umekuwa ukisuasua bila sababu za wazi.
Alitaka kujua mkakati rasmi wa halmashauri katika kuwaandaa vijana hao kisaikolojia na kiutaratibu ili wawe tayari kuhamia maeneo mapya pale itakapohitajika kufanya hivyo.
Alionya kuwa manispaa isipoanza kuchukua hatua mapema, shughuli hizo zinaweza kuwa chanzo cha migogoro na usumbufu mkubwa siku za usoni, hasa wakati wa kupanga upya matumizi ya ardhi katika eneo hilo.
Katika majibu ya awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa alisema kuwa uongozi wa manispaa ulihakikishia baraza kuwa suala hilo litashughulikiwa kwa umakini na kwa kushirikiana na pande zote husika.
Alisema mpango unaoendelea ni kuendelea kuwahamasisha vijana kutafuta maeneo mbadala, huku jukumu la halmashauri likiwa ni kuweka mazingira bora ya biashara bila kuathiri usalama, mpangilio wa mji na matumizi sahihi ya miundombinu.
Meya wa Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada alisema kuwa masuala yote yaliyotajwa yanahitaji utekelezaji wa haraka na ushirikiano wa taasisi zote za serikali, wadau na wananchi, ili kuboresha huduma, kukuza uchumi wa manispaa na kuhakikisha mazingira salama na yenye mpangilio kwa wote.

