Mkurugenzi wa Shughuli za Baraza la Wawakilishi Othman Ali Haji akitoa Taarifa kwa Vyombo vya Habari mbalimbali kuhusiana na Kuanza kwa Kikao cha Baraza la Wawakilishi Tarehe 06 May 2026,amabapo jumla ya Maswali 506 yakiwemo yale yaliobaki katika Kikao Kilichopita na yasasa yataulizwa ,hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Baraza hilo Chukwani Zanzibar.
Mkurugenzi Idara ya Ushauri wa Kisheria Baraza la Wawakilishi Nasra Awadh akifafanua baadhi ya Maswali yalioulizwa na Waandishi a Habari katika Mkutano kuhusiana na Taarifa ya Kuanza kwa Kikao cha Baraza la Wawakilishi Tarehe 06 May 2026,amabapo jumla ya Maswali 506 yakiwemo yale yaliobaki katika Kikao Kilichopita na yasasa yataulizwa .Taarifa iliotolewa na Mkurugenzi wa Shughuli za Baraza la Wawakilishi Othman Ali Haji ,hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Baraza hilo Chukwani Zanzibar.
Baadhi ya Waandishi wa Habari waliohudhuria katika Mkutano kuhusiana na Taarifa ya Kuanza kwa Kikao cha Baraza la Wawakilishi Tarehe 06 May 2026,amabapo jumla ya Maswali 506 yakiwemo yale yaliobaki katika Kikao Kilichopita na yasasa yataulizwa .Taarifa iliotolewa na Mkurugenzi wa Shughuli za Baraza la Wawakilishi Othman Ali Haji ,hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Baraza hilo Chukwani Zanzibar.
…………….
Mkutano wa Tatu wa Baraza la Kumi na Moja la Wawakilishi unatarajiwa kuanza rasmi Jumatano, Mei 6, 2026, ukiwa na ajenda ya majadiliano ya Bajeti ya Serikali pamoja na masuala mbalimbali.
Taarifa hiyo iliwasilishwa na Mkurugenzi wa Shughuli za Baraza, Othman Ali Haji, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Baraza la Wawakilishi, wakati akizungumshwa na waandishi wa habari Katika mkutano uliofanyika Katika Baraza Hilo Chukwani Zanzibar.
Akieleza kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Othman alisema Ofisi ya Baraza imepokea jumla ya maswali 459 mapya kutoka kwa wajumbe, sambamba na maswali yaliyobakia kutoka mkutano uliopita, hali inayofanya idadi ya maswali yatakayojadiliwa kufikia 506.
Kwa upande wa Bajeti, majadiliano yataanza kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, kabla ya kuendelea na wizara na taasisi nyingine za Serikali.
Aidha, alieleza kuwa Baraza litajadili Bajeti Kuu ya Serikali Kwa mwaka wa fedha 2026/2027 pamoja na kuwasilisha na kujadiliwa kwa miswada miwili ya sheria ikiwemo Mswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2026 na Mswada wa Sheria ya Makadirio ya Matumizi kwa mwaka huo wa fedha.
Katika hatua nyingine, mkutano huo pia utapokea taarifa ya Serikali kuhusu hali ya dawa za kulevya Zanzibar, jambo linalotarajiwa kuchochea mjadala mpana kuhusu athari na mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo katika jamii.
Akizungumzia ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkurungezi Idara ya ushauri wa kisheria Nasra Awadhi salmini alieleza kuwa utaratibu wa kanuni za Baraza unaelekeza Serikali kuwasilisha kauli rasmi kuelezea yaliyomo katika ripoti hizo baada ya kupokelewa na Rais.
Baada ya hapo, Waziri husika hupata fursa ya kuwasilisha maelezo, huku wajumbe wakipewa nafasi ya kuuliza maswali kabla ya ripoti hizo kukabidhiwa Kamati ya Hesabu za Serikali kwa uchambuzi na mapendekezo.
Aliongeza kuwa ripoti za mwaka jana zilipokelewa na zinaendelea kufanyiwa kazi, huku za mwaka huu tayari zimewasilishwa kwa hatua zinazofuata za kikanuni.
“Mchakato wa kujadili ripoti hizo unatekelezwa kwa mujibu wa kanuni, ambazo zinaelekeza kujadiliwa kwake katika mwezi wa Februari, kama sehemu ya utaratibu wa kuimarisha uwazi na uwajibikaji serikalini.” Alisema Nasra.