Na Silivia Amandius 

Kagera.

Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa majiko banifu nchini, ambapo jumla ya majiko 200,000 yatasambazwa kote Tanzania ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Mkoa wa Kagera umepata jumla ya majiko 12,000 yatakayogawiwa katika halmashauri saba.

Kwa mujibu wa mgawanyo huo, Halmashauri ya Biharamulo itapata majiko 1,854, huku halmashauri nyingine ambazo ni Muleba, Bukoba Vijijini, Missenyi, Ngara, Kyerwa na Karagwe kila moja ikipata majiko 1,853.

Akizungumza kuhusu mradi huo, Mhandisi Mwandamizi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Deusdedit Malulu, amesema kuwa kila mwananchi atanunua jiko moja kwa bei ya ruzuku ya shilingi 12,500 badala ya zaidi ya shilingi 60,000. Ameongeza kuwa mradi huo una lengo la kutekeleza agizo la Rais la kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia. Mradi huo umegharimu takribani shilingi milioni 700.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Kitengo cha Biashara na pia msimamizi wa masuala ya nishati safi ya kupikia, Ndugu Issaya Tendega, amesema kuwa taasisi zenye watu zaidi ya 100 zinatakiwa kutumia nishati safi ya kupikia. Amebainisha kuwa baadhi ya taasisi kama magereza, vyuo vya VETA na shule kadhaa mkoani Kagera tayari zimeanza kutumia nishati hiyo.

Aidha, Tendega amewataka wasambazaji wa majiko hayo kuhakikisha kunakuwa na uwiano sawa katika ugawaji kwa halmashauri zote, huku akiipongeza REA kwa juhudi zao za kuendelea kutoa huduma na elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Ndugu Stephen Ndaki, aliyepokea majiko hayo kwa niaba ya wananchi, amesema usambazaji wake utafanyika vijijini ndani ya siku 15 hadi 20. Majiko hayo yatasambazwa na kampuni ya BURN Manufacturing, kupitia mwakilishi wake Ndugu John Mtui.

Imeelezwa kuwa ili kupata jiko hilo, mwananchi atalazimika kuwa na namba ya NIDA ili kuzuia mtu mmoja kupata zaidi ya jiko moja. Majiko hayo yanakadiriwa kudumu zaidi ya miaka mitano na yana faida kubwa katika kuhifadhi mazingira kwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Mradi huu unatarajiwa kuwa suluhisho muhimu katika kupunguza uharibifu wa mazingira na kuboresha afya za wananchi kupitia matumizi ya nishati safi ya kupikia.