Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru(TAMCU LTD)Mussa Manjaule kushoto na meneja masoko wa benki ya CRDB Kanda ya kusini Emanuel Biganio,wakibadilishana hati za makabidhiano ya magari matano aina ya Howo yaliyonunuliwa na chama hicho kupitia mkopo uliotolewa na CRDB,katikati Mkuu wa wilaya ya Tunduru Denis Masanja

……………

Na Mwandishi Wetu, Tunduru

BENKI ya CRDB, imekabidhi malori matano mapya aina ya HOWO kwa chama kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma(TAMCU LTD) kwa ajili ya kubeba mazao ya wanachama na wakulima wengine wanaohudumiwa na chama hicho na kuwa chanzo cha mapato ya chama.

Meneja wa benki ya CRDB Tawi la Tunduru Emanuel Mwasuka alisema,magari hayo yana thamani ya Sh.blioni 1.5 ambapo kati ya fedha hizo CRDB imetoa cha Sh.735 na Chama kikuu kimechangia Sh.milioni 315.

Alisema,CRDB itaendelea kutoa mikopo ya fedha kwa vyama vikuu na vyama vya msingi vya ushirika(Amcos)vyenye mahitaji kwani uchumi wa wilaya ya Tunduru unaendelea kukua kwa kasi kubwa huku mahitaji ya magari kwa ajili ya kubeba mazao na bidhaa nyingine ikiongezeka.

Amewataka viongozi wa Tamcu na wanachama wa chama hicho,kuyatunza magari hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu na kufanya kazi iliyokusudiwa ya kuongeza mapato ya chama ili kuleta tija kwa chama na wanachama.

“Magari haya ni chanzo kikubwa cha mapato kwa chama kikuu,hii ni fursa kubwa na mfano mzuri kwa vyama vingine vikuu katika mkoa wetu wa Ruvuma na mikoa jirani,ninavyokitazama chama kikuu Tamcu kitafika mbali zaidi na benki ya CRDB itaendelea kutoa mikopo kama kuunga mkono jitihada zao”alisema Mwasuka.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tunduru Denis Masanja,amekipongeza Chama kikuu kununua malori hayo ambayo yatapunguza kero ya kusafirisha mazao ya wakulima kutoka mashambani na kupeleka kwenye maghala ya vyama vya msingi vya ushirika.

Alisema,malori hayo ni hatua kubwa katika sekta ya usafirishaji,kuongeza ufanisi wa biashara ya korosho,ufuta na mbaazi mazao yanayolimwa kwa wingi na kuuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani,kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza tija kwa wanachama.

“Haya ni maendeleo makubwa katika sekta ya ushirika,nawaomba wanachama muwape ushirikiano viongozi wa Tamcu hususani mwenyekiti,wajumbe wa bodi na watumishi ili waendeleaa kufanya mambo makubwa zaidi kwa manufaa yenu wanachama na wakulima”alisema Masanja.

Akizungumza kwa niaba ya ya wakulima wengine Rashid Chibwana,amekipongeza chama kikuu cha ushirika(TAMCU)kwa kununua magari makubwa mapya matano ya kubebea mizigo ambayo yatasaidia kupunguza adha ya kuchelewesha mazao yao kwenda mnadani na kushindwa kupata fedha kwa wakati.

Chibwana alisema,magari hayo yatarahisisha na kutumikia wakulima kwa kuwafikia walipo kwa ajili ya kusafirisha mazao kutoka mashambani na kupeleka kwenye maghala kabla ya kuuzwa kwenye minada.

“Tunawashuru sana viongozi wa chama chetu Tamcu kwa kuongeza miradi ya chama chetu,huko nyuma tulitegemea chanzo kimoja tu cha mapato ambacho ni ushuru,lakini magari haya yatakuwa chanzo kikubwa cha mapato na kurahisisha usafirishaji wa mazao yanayolimwa na kukusanywa na vyama vyetu kutoka kwa wakulima”alisema Chibwana.

Alisema, katika wilaya ya Tunduru kuna uhaba mkubwa wa magari ya kubebea mazao na yaliyopo ni mabovu hivyo yanashindwa kufikisha mazao kwenda kwenye maghala ya chama kikuu kwa wakati.

Naye Mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika(Tamcu)Mussa Manjaule alisema,ununuzi wa magari hayo ni utekelezaji wa maagizo ya wanachama ambao waliitaka bodi ya chama hicho kununua magari ya mizigo ili yasaidia kubeba mazao na kuwa chanzo cha mapato.

Manjaule alisema,awali walikuwa wanapata shida kuleta viuatilifu kutoka mkoa jirani wa Mtwara kuleta Tunduru kwa ajili ya wakulima,lakini kwa sasa magari hayo yatakuwa mkombozi kwa wanachama na wakulima wengine wa wilaya hiyo.