NA DENIS MLOWE, IRINGA 
MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM, Festo Shem Kiswaga, ambaye anatoka katika eneo la Iringa Vijijini, leo amezungumza na waandishi wa habari na kutoa taarifa ndefu kuhusu mwenendo wa mchakato wa uchaguzi wa ndani wa Chama Cha Mapinduzi katika Jimbo la Isimani.
Akizungumza Kiswaga alisema kuwa amehudumu kama mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kwa takribani miaka kumi na tano, na pia amewahi kuwa mtendaji wa serikali hadi ngazi ya wilaya, uzoefu ambao anasema umemjengea uelewa mpana wa taratibu za chama na serikali.
Kiswaga alianza kwa kutoa shukrani zake za dhati kwa viongozi wa chama ngazi ya wilaya, akiwemo mwenyekiti wa CCM wilaya, kamati ya siasa ya wilaya, na katibu wa chama, kwa usimamizi wao makini katika zoezi la kura za maoni. 
Pia aliwapongeza viongozi wa ngazi ya mkoa kwa weledi na uwazi waliouonyesha katika usimamizi wa mchakato, akiwataja viongozi hao kama sehemu muhimu ya kuimarisha demokrasia ndani ya chama.
Aidha, aliwashukuru viongozi wa taifa akiwemo Mwenyekiti wa CCM Taifa, Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha kuwa mchakato wa kupata mgombea wa jimbo la Isimani unafanyika kwa kuzingatiia sifa, weledi na utendaji wa kila mgombea.
Kiswaga alibainisha kuwa katika mchakato huo kulikuwa na wagombea kumi na nane, lakini hatimaye jina moja lilipenya na kupitishwa na vikao halali vya chama, ambapo Bi. Emanuela Mtatifikolo Kaganda aliteuliwa kupeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi katika jimbo hilo. Bi. Kaganda, ambaye kwa sasa alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Babati, amesifiwa mno na Kiswaga kwa utendaji wake.
Kiswaga alieleza kuwa anamfahamu vizuri Emanuela Kaganda kwa kuwa walifanya kazi kwa karibu wakati yeye akiwa DC wa Monduli na Kaganda akiwa DC wa Babati. Alisema kuwa ameshuhudia kwa macho yake uchapa kazi wa Kaganda, uwezo wake wa kusimamia miradi, na weledi wake katika kuongoza watu.
Aliendelea kufafanua kuwa Bi. Kaganda ni msomi, jasiri, na mtu mwenye historia ndefu ya kulitumikia chama na serikali.
 Aliongeza kuwa uteuzi wake ni ushahidi kwamba chama kinathamini utendaji bora na uwajibikaji.
Katika hotuba yake, Kiswaga alisema kuwa mara tu baada ya kutangazwa kwa uteuzi huo, alimpigia simu Kaganda ili kumpongeza.
 Alimwambia kuwa amestahili nafasi hiyo kwa sababu ya sifa zake tatu kuu ikiwemo uadilifu, utendaji mzuri na uwezo wa kusimamia maendeleo katika maeneo aliyowahi kuongoza.
Kiswaga pia alitoa wito kwa wananchi wa Isimani kuungana na kumuunga mkono mgombea huyo, akisema kuwa eneo hilo limepata kiongozi mahiri, muadilifu na mchapakazi, ambaye anaweza kulisukuma mbele kimaendeleo na kuliletea heshima ndani ya chama na taifa.
Aidha, aliwashukuru wanachama wa CCM na wote waliojitokeza kwenye mchakato wa kura za maoni, akiwataka kuendelea kuwa wamoja bila kujali matokeo, kwani lengo kuu ni kuona chama kinaendelea kushinda na kuongoza wilayani, mkoani na kitaifa.
Kwa ujumla, Kiswaga alihitimisha kwa kusisitiza kuwa uteuzi wa Emanuela Kaganda ni hatua muhimu kwa mustakabali wa Jimbo la Ismani na chama kwa ujumla, na akasisitiza kuwa yuko tayari kushirikiana na mgombea huyo katika kampeni kuanzia uzinduzi hadi ufungaji wa kampeni kuhakikisha chama kinashinda.