Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, akizungumza jambo leo Mei 3, 2026  wakati akikagua  maendeleo ya mradi wa nyumba 144 unaotekelezwa na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) katika Manispaa Temeke, Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Daud Kondoro akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa nyumba 144 unaotekelezwa na TBA Manispaa ya Temeke.

Muonekano wa mradi wa nyumba 144 unaotekelezwa na TBA, Manispaa ya Temeke.

……………

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Serikali imeanza kuelekeza nguvu katika kutatua changamoto ya makazi kwa vijana kwa kujenga nyumba za gharama nafuu katika jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo Mei 3, 2026 l, Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, alipokagua maendeleo ya mradi wa nyumba 144 unaotekelezwa na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA), Wilayani Temeke.

Mhe. Ulega amesema kuwa kipaumbele katika mradi huo ni vijana walioanza ajira na wale wanaojiajiri, hatua inayolenga kuwasaidia kuondokana na adha ya kuishi mbali na maeneo yao ya kazi kutokana na uhaba wa nyumba nafuu.

Amesema kuwa serikali inaamini kuwakaribisha vijana karibu na fursa za ajira, itaongeza ufanisi wao kazini na kupunguza muda wanaopoteza katika usafiri na utafutaji wa makazi.

“Katika mradi huo, jumla ya nyumba 144 zinajengwa, zikiwemo 72 za chumba kimoja pamoja na sebule, jiko na choo, na nyingine 72 zikiwa na vyumba viwili, kimoja kikiwa na huduma kamili (self-contained), pamoja na sebule, jiko na choo cha pamoja” amesema Mhe. Ulega.

Waziri Ulega amebainisha kuwa mpango huo si wa Dar es Salaam pekee, bali umeidhinishwa pia kupanuliwa katika mikoa mingine ikiwemo Dodoma, kwa ridhaa ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Lengo kuu ni kupunguza pengo kubwa la makazi lililobainishwa tangu Sensa ya mwaka 2020.

Aidha, amesisitiza kuwa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ni sehemu ya mkakati mpana wa kitaifa uliopo ndani ya Dira ya Taifa 2050, unaolenga kuhakikisha Watanzania, hususan vijana, wanapata makazi bora kwa bei nafuu kulingana na mahitaji ya maeneo mbalimbali nchini.