Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza ujio wa viongozi wawili wa Afrika Mashariki, Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto, wanaotarajiwa kufanya ziara rasmi nchini Mei, 2026 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kidiplomasia na kiuchumi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Rais Kagame anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi tarehe 03 Mei, 2026 ambapo atapokelewa rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa viongozi hao watakuwa na mazungumzo rasmi yatakayolenga kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji, miundombinu, kilimo, afya, elimu na nishati, pamoja na kudumisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Rwanda.

Aidha, Rais Kagame anatarajiwa kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma kabla ya kuhitimisha ziara yake na kurejea nchini Rwanda.

Kwa upande mwingine, Rais wa Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto, anatarajiwa kuanza ziara ya kitaifa nchini tarehe 04 na 05 Mei, 2026 ambapo atapokelewa rasmi na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Ruto atafanya mazungumzo ya pande mbili na mwenyeji wake kabla ya viongozi hao kuzungumza na vyombo vya habari na kushuhudia utiaji saini wa mikataba na hati mbalimbali za ushirikiano.

Jioni ya siku hiyo, Rais Ruto anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake, kabla ya kuelekea jijini Dodoma tarehe 05 Mei, 2026 kwa ajili ya kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, pamoja na ratiba nyingine, Rais Ruto ataungana na Rais Samia katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Kenya litakalofanyika jijini Dar es Salaam, likilenga kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kuvutia uwekezaji wa pamoja.

Serikali imeeleza kuwa ziara hizi zinatarajiwa kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania, Rwanda na Kenya, huku zikichochea maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa wananchi wa nchi hizo.

Kwa pamoja, nchi hizi zimeendelea kushirikiana kwa karibu kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambapo kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo Tume ya Pamoja (JPC), zimefanikiwa kuimarisha biashara na uwekezaji katika sekta nyingi.

Aidha, taarifa hiyo imebainisha kuwa katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2024, biashara ya bidhaa kati ya Tanzania, Kenya na Rwanda imeendelea kuongezeka kwa kasi, huku ikichangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi hizo na ajira kwa wananchi wake.

Vilevile, Tanzania imekuwa ikiendelea kuuza bidhaa mbalimbali nchini Rwanda na Kenya, huku kila nchi ikiwekeza katika uchumi wa mwenzake, hatua inayochochea ustawi wa pamoja wa kanda ya Afrika Mashariki.

Serikali imewataka wananchi na vyombo vya habari kuzipokea ziara hizo kwa ushirikiano na kuendelea kudumisha amani na utulivu, huku ikisisitiza dhamira ya nchi hizo kuendeleza na kuimarisha mshikamano wa kikanda.