NA DENIS MLOWE IRINGA
KIJANA mzalendo Alphonce Myinga, maarufu Black, ameendeleza jitihada za kuhamasisha uzalendo kupitia hatua ya kuwagawia mafuta zaidi ya vijana 100 wa bodaboda katika mji wa Iringa. Zoezi hilo limefanyika katika maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi, likilenga kuhimiza ushiriki wa vijana katika kulinda amani ya taifa.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Black alisema amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kuwaelimisha vijana kuhusu thamani ya uzalendo. Alieleza kuwa juhudi zake ziliungwa mkono na mdau mmoja aliyeguswa na kazi yake na kutoa mchango wa shilingi milioni moja kwa ajili ya kuendeleza kampeni ya kuhamasisha amani.
Alisema kuwa aliamua kuelekeza fedha hizo kwa vijana wa bodaboda kutokana na nafasi yao muhimu katika jamii, ikiwemo kukutana na watu wengi kila siku na hivyo kuwa na uwezo wa kueneza ujumbe wa amani na mshikamano. Black alibainisha kuwa ameanza kampeni hiyo mkoani kwao Iringa, huku akipanga kuisambaza maeneo mengine nchini ili kuwafikia vijana wengi zaidi.
Akitoa wito kwa vijana, Black aliwasisitiza kuwa makini dhidi ya watu au makundi yanayoweza kuchochea chuki au vurugu. Alisema kuwa Tanzania ni nchi yenye umoja na mshikamano, na amani iliyopo haina mbadala. Alionya kuwa madhara ya kuvuruga amani ni makubwa na humgusa kila mwananchi.
Aidha, aliwahimiza vijana kuunga mkono juhudi za serikali katika kuleta maendeleo, akieleza kuwa utulivu wa nchi ndiyo msingi wa mafanikio hayo. Alisema kuwa hatua zinazochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kielelezo cha dhamira ya kujenga taifa bora, hivyo zinahitaji ushirikiano wa vijana na wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodaboda mkoani Iringa, Zuberi Mapilla, alimpongeza Black kwa msaada huo akisema umeleta faraja kwa vijana hususan kutokana na changamoto ya kupanda kwa bei ya mafuta. Alisema kwamba zaidi ya msaada huo, ujumbe wa kuhimiza amani ni muhimu kwa ustawi wa vijana na taifa. Mapilla aliongeza kuwa hatua hiyo imeonyesha kuwa uzalendo unaweza kuonekana kupitia matendo yanayogusa maisha ya watu moja kwa moja na kwamba imeacha alama ya matumaini kwa vijana wengi.

