Baadhi ya wafanyakazi wa mkoa wa Katavi.

……………… 

Na. Mwandishi wetu Katavi

Mkuu wa mkoa wa katavi bi. Mwanamvua Mrindoko ametoa siku thelathini kwa taasisi zote za umma zikiwemo halmashauri kuhakikisha madai yote ya watumishi wa ajira mpya yanalipwa na kuwataka waajiri wanaochelewesha stahiki za wafanyakazi wao kwa makusudi kuhakikisha wanawalipa wafanyakazi hao.

Mkuu huyo wa mkoa wa Katavi ametoa agizo hilo wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi kimkoa yaliyyofanyika katika uwanja wa kashaulili katika Manispaa ya Mpanda.

“Zipo halmashauri ambazo kwa makusudi zinatafuta visingizio mara vya mtandao uko chini, mara hivi mara vile na kushindwa kulipa wakati bajeti tayari imepitisha” alisema Mrindoko.

Aidha alimtaka katibu tawala wa mkoa wa Katavi kufuatilia suala hilo na kumpa taarifa baada ya siku thelathini.

“Nione huyo asiyetaka kulipa ndio atajua atakachokipata! Mnasababisha manung’uniko yasiyo ya lazima kwa watumishi wenu” aliongeza.

Pia aliwataka watumishi kuendelea kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa ushirikiano kwa ajili ya kuuendeleza mkoa wa Katavi.

Awali akisoma risala ya wafanyakazi iliyoandaliwa na TUKTA Katibu wa CWT halmashauri ya Nsimbo Phineas Sogoti alisema watumishi wa ajira mpya wanapitia changamoto kadhaa ikiwemo kucheleweshewa madai yao.

Changamoto nyingine alizosema zinaathiri wafanyakazi kwa ujumla ni pamoja na kikotoo kwani kinawanyima usingizi.