Na.Sophia Kingimali
Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Prof. Said Mohammed, ametangaza rasmi kuanza kwa mitihani ya taifa ya kidato cha sita na ualimu kwa mwaka 2026, huku akisisitiza amani na utulivu katika kipindi chote cha mitihani hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 3,2026 jijini Dar es Salaam, Prof. Mohammed amesema mitihani hiyo itaanza Mei 4, 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara, ambapo mitihani ya ualimu itakamilika Mei 18 huku ya kidato cha sita ikihitimishwa Mei 25 mwaka huu.
Amefafanua kuwa mtihani wa kidato cha sita utafanyika katika shule za sekondari 1,068 pamoja na vituo 226 vya watahiniwa wa kujitegemea, wakati mtihani wa ualimu utafanyika katika vyuo 104 vya ualimu nchini.
Kwa upande wa usajili, jumla ya watahiniwa 133,655 wamejiandikisha kufanya mtihani wa kidato cha sita, ambapo kati yao watahiniwa wa shule ni 126,578 na wa kujitegemea wakiwa ni asilimia 77. Kati ya watahiniwa wa shule, wavulana ni asilimia 51 huku wasichana wakiwa asilimia 49, takwimu inayoonesha uwiano mzuri wa kijinsia.
Aidha, watahiniwa wa mtihani wa ualimu waliojiandikisha ni 14,679, ambapo 12,789 watafanya mtihani kwa mara ya kwanza kulingana na mtaala ulioboreshwa, huku wengine wakifanya marudio kwa kutumia mtaala wa zamani.
Dk Mohammed amesema NECTA imekamilisha maandalizi yote muhimu ikiwemo usambazaji wa mitihani, vijitabu vya kujibia na kuendesha mafunzo kwa wasimamizi ili kuhakikisha mitihani inafanyika kwa utulivu, usalama na uadilifu wa hali ya juu.
Pia amebainisha kuwa watahiniwa wenye mahitaji maalum 214 kwa kidato cha sita na 42 kwa ualimu wametambuliwa na kuandaliwa mazingira rafiki, ikiwemo mitihani ya maandishi yaliyokuzwa na muda wa nyongeza kulingana na mahitaji yao.
Ametoa wito kwa wasimamizi, walimu, wazazi na jamii kwa ujumla kushirikiana kulinda uadilifu wa mitihani, akisisitiza kuwa NECTA haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayehusika na udanganyifu, ikiwemo kufuta matokeo au kituo cha mtihani.
Kwa upande wa watahiniwa, amewahimiza kuzingatia maelekezo yote na kuepuka vitendo vya udanganyifu, akisisitiza kuwa mitihani hiyo ni kipimo muhimu cha maarifa na msingi wa kuchagua wanafunzi watakaojiunga na elimu ya juu pamoja na taaluma mbalimbali nchini.

