Zaidi ya wananchi 15,000 wa Baray wanatarajiwa kunufaika na huduma ya maji safi na salama kufuatia uzinduzi wa mradi mkubwa wa maji uliofanywa na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, aliyesisitiza kuwa upatikanaji wa maji ni haki ya msingi na nguzo muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhandisi Kundo amesema ni heshima kubwa kwake kushiriki katika hafla hiyo kwa niaba ya Waziri wa Maji, akibainisha kuwa miradi ya maji ina nafasi ya kipekee katika kubadilisha maisha ya wananchi, hasa wa maeneo ya vijijini, kwa kuwa huongeza upatikanaji wa huduma muhimu na kuboresha ustawi wa jamii.

Katika hotuba yake, ametoa shukrani kwa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa uwekezaji wao katika sekta ya maji, akieleza kuwa huu ni mradi wa 30 walioutekeleza nchini ndani ya kipindi cha muongo mmoja, ukiwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.5 zilizolenga kuboresha maisha ya wanachi. Aliwapongeza pia Africai kwa kujitoa katika kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo unafanikiwa. 

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele kikubwa katika kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama, akieleza kuwa tayari huduma hiyo imefikia asilimia 85.2 vijijini, huku jitihada zikiendelea kufikia vijiji vyote vilivyosalia ifikapo mwaka 2030.

Mhandisi Kundo pia amepongeza mchango wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa kusimamia miradi hiyo na kuhakikisha inakuwa endelevu, sambamba na kuipongeza SBL na Africai kwa kutekeleza programu ya kuwawezesha wanawake 30 kupitia mafunzo ya uongozi, ujasiriamali na elimu ya fedha.

Akihitimisha, amewataka wananchi wa Baray kulinda na kuthamini miundombinu ya maji, kushirikiana na vyombo vya watumia maji katika usimamizi wake, na kutumia rasilimali hiyo kuboresha maisha yao, huku akiitaka sekta binafsi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo endelevu nchini.