▪️Waziri Mavunde Asisitiza Ushirikiano wa Kikanda
▪️Ahimiza Uwekezaji Miundombinu ya Kisaaa, Nishati na Sera Rafiki
▪️Azishauri Serikali Kufanya Kazi kwa Ukaribu na Sekta Binafsi
Nairobi, Kenya
Serikali ya Tanzania imetoa msimamo thabiti wa kuitaka Afrika kuharakisha mageuzi ya Sekta ya Madini kwa kuwekeza katika uongezaji thamani wa rasilimali zake zikiwemo za madini badala ya kuendelea kuuza madini ghafi yasiyoongeza tija kwa uchumi wa bara hilo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini wa Tanzania Mhe. Anthony Mavunde wakati akifunga Mkutano wa Kenya Mining Investment Conference & Expo 2026 jijini Nairobi, uliofanyika kwa siku mbili kuanzia Aprili 28 hadi 29, 2026, ambako amesema hatua ya kuchakata madini ndani ya nchi ni nguzo muhimu ya kujenga uchumi wa viwanda na kuongeza ushindani wa Afrika katika soko la dunia.
“Afrika haiwezi kuendelea kusafirisha malighafi ghafi na kuagiza bidhaa zilizokamilika. Tunapaswa kujenga uwezo wa kuchakata na kuongeza thamani ya madini yetu hapa hapa nyumbani,” amesisitiza Waziri Mavunde
Ameeleza kuwa ili kufanikisha azma hiyo, nchi za Afrika zinapaswa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa, nishati ya uhakika na sera rafiki zitakazovutia uwekezaji katika viwanda vya uchakataji madini.
Akizungumzia uwekezaji, Mhe. Mavunde amebainisha kuwa uwepo wa mitaji na teknolojia pekee hautoshi, bali mazingira yenye kuaminika ndiyo kichocheo kikuu cha kuvutia wawekezaji. Amesisitiza umuhimu wa uthabiti wa sera, uwazi katika utoaji wa leseni pamoja na mifumo ya kodi inayotabirika.
Aidha, amezitaka Serikali za Afrika kubadili mtazamo na kuwa washirika wa moja kwa moja katika maendeleo ya Sekta ya Madini kwa kusaidia kupunguza hatari katika miradi mikubwa, kuwezesha upatikanaji wa mitaji na kuendeleza miundombinu.
Katika kuimarisha ushindani wa bara hilo, Waziri Mavunde amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda akieleza kuwa Afrika itapata nguvu zaidi ikiwa nchi zake zitaunganisha rasilimali na kujenga mifumo ya pamoja ya uchakataji na masoko.
Kwa upande wa jamii, amekumbusha kuwa mafanikio ya Sekta ya Madini yanapaswa kwenda sambamba na ustawi wa wananchi kupitia ajira, ulinzi wa mazingira na maendeleo ya kiuchumi ya maeneo yanayozunguka migodi.
Akihitimisha, Mhe. Mavunde amesema mahitaji ya madini muhimu duniani yanaongezeka kwa kasi, hivyo Afrika ina nafasi ya kipekee ya kunufaika ikiwa itachukua hatua za haraka na za kimkakati.
“Huu ni wakati wa Afrika kuchukua hatua za pamoja ili kuhakikisha rasilimali zake zinawanufaisha wananchi wake na kuijenga kuwa kitovu cha viwanda na uchumi wa kisasa,” amesisitiza Waziri Mavunde.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Uchumi wa Bluu na Masuala ya Bahari wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Hassan Ali Joho, amesisitiza kuwa Sekta ya Madini nnchni Kenya itaendelea kujifunza usimamizi na uendeshaji madhubutiwa sekta hiyo kutoka Tanzania kwa hatua walizochukua kufikia hatua hiyo na kwamba Sekta ya Madini Kenya imewekewa lengo la kuchangia aslimia 10 katika Pato la Taifa (GDP) kufikia mwaka 2030.
Mkutano huo umewakutanisha viongozi wa Serikali, wawekezaji na wadau wa Sekta ya Madini kutoka ndani na nje ya Afrika kujadili fursa na changamoto za maendeleo ya sekta hiyo, huku Tanzania iking’ara zaidi kwa mijadala kwa mafanikio yake katika Sekta hiyo kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.





