Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha elimu ya upandaji miti inatolewa kwa wanachi hususan wale wa vijijini ili waweze kushiriki vizuri katika biashara ya kaboni.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Dkt. Festo Dugange wakati akijibu maswali kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais bungeni jijini Dodoma leo Aprili 30, 2026.
Katika swali lake Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Maryam Azan Mwinyi alitaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu ya upandaji miti ili wananchi hasa wale wa vijijini washiriki katika biashara ya kaboni.
Akijibu swali hilo, Dkt. Dugange alifafanua kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeendelea kutekeleza kampeni za upandaji miti katika halmashauri zote nchini.
Alisema pia, vimeratibiwa vipindi vya redio na televisheni ikiwemo kipindi cha Mazingira yetu na Tanzania Tuitakayo kinachorushwa kila Jumatatu kupitia TBC ambapo elimu ya upandaji miti na biashara ya kaboni hutolewa.
Naibu Waziri huyo alitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa TFS kila kanda kusambaza miche kwa wananchi kwa ajili ya kuipanda katika maeneo yao na kuitunza, hatua itakayosaidia uhifadhi wa mazingira kuwa endelevu.
Aidha, Dkt. Dugange alieleza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuwajengea uwezo maafisa mazingira katika ngazi ya Serikali za Mitaa kuhusu umuhimu wa upandaji miti na fursa ya biashara ya kaboni ili kuhakikisha wananchi wote wanashiriki katika biashara hiyo.
Kwa upande mwingine alisema Serikali imetoa elimu kwa makundi yenye ushawishi katika jamii ikiwemo kundi la wabunge ili wawe chachu ya kuhamisisha wananchi katika upandaji miti na kushiriki kikamilifu katika biashara ya kaboni.
Pia, Dkt. Dugange alisema kuwa Serikali itaendelea na jitihada za kutoa elimu kwa jamii ili waweze kunufaika ipasavyo na biashara ya kaboni kupitia Kituo cha Kuratibu Kaboni (NCMC).
Alisema kituo hicho tayari kina Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti yake ambayo imeanza majukumu yake rasmi yakiwemo kutoa miongozo ili wananchi kupitia halmashauri zao waweze kunufaika.




