Na WMJJWM – Iringa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amesisitiza kuwa maendeleo ya jamii hayawezi kuletwa na Serikali pekee, bali yanahitaji ushiriki wa wananchi wanaotumia fursa zilizopo kujiongezea ujuzi na kutatua changamoto zinazowazunguka.
Akizungumza Aprili 28, 2026 katika hafla ya utoaji vyeti kwa wahitimu 40 wa fani ya ushonaji na usanifu wa mavazi katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Rungemba mkoani Iringa, Dkt. Jingu amewahimiza vijana kuchangamkia mafunzo ya vitendo ili kujenga uwezo wa kujiajiri na kupunguza tatizo la ajira nchini.
“Sekta ya ubunifu wa mavazi ina nafasi kubwa ya kukuza kipato, kuwa mbunifu, uamunifu na weledi, tumieni mitandao ya kijamii kutangaza kazi zenu hii itaongeza thamani katika bidhaa mnazazozalisha” amesema. Dkt. Jingu.
Dkt. Jingu amewakabidhi wahitimu hao vyerehani ikiwa ni nyenzp muhimu ya kuanzia kufanya kazi Ili waweze kujiendeleza na kukuza Kasi zao na kujipatia kipato.
Aidha, amewahamasisha vijana kuangalia fursa zilizopo katika maeneo yao ikiwemo kuchangamkia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ili kuanzisha au kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo hicho, Kidubya Busanji, amesema Chuo hicho kitaendelea kutoa hamasa kwa wananchi kujiunga na mafunzo mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za kijamii kupitia ujuzi.
Ameongeza kuwa Chuo hicho kitaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha makundi yote ya jamii, hususan vijana na wanawake, wanapata fursa ya kujifunza na kujiajiri.





