Na Mwandishi Wetu
Shirika la Mawasiliano Tanzania, TTCL, limesema linaendelea kuboresha huduma zake kwa wateja baada ya kununua magari saba aina ya Hilux na bajaji 28 kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi wa idara ya ufundi.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya shirika hilo kupata faida ya Shilingi bilioni 22.98 katika mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo kati ya fedha hizo limetumia Shilingi bilioni 1.6 kununua magari na Shilingi milioni 291.2 kwa ajili ya bajaji hizo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa makabidhiano ya vitendea kazi hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, amesema hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi kwa kuwafikia wateja kwa wakati.
Amesema magari na bajaji hizo zitatumika kuwahudumia wateja wanaopata changamoto katika matumizi ya huduma mbalimbali za TTCL ikiwemo huduma ya Faiba Mlangoni.
“Magari pamoja na bajaji hizi zitatumiwa na mafundi na watumishi wanaohudumia wateja, pindi huduma zinapokatika au wateja wanapopata hitilafu, mafundi wetu watawafikia kwa wakati na kutatua changamoto hizo kwa ufanisi zaidi,” amesema Marwa.
Aidha, amesema shirika hilo limepanga kupokea magari mengine matano aina ya Hiace mwishoni mwa mwezi huu, ambayo yatatumika katika shughuli za masoko na mauzo ili kuwafikia wateja wengi zaidi.
Amesema ununuzi wa vitendea kazi hivyo umetokana na faida iliyopatikana na unalenga kuimarisha huduma, kuongeza mapato ya shirika pamoja na kuchangia gawio kwa Serikali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi wa TTCL, Mhandisi Cecil Francis, amesema hatua hiyo ni ya kimkakati katika kuboresha utoaji wa huduma za mawasiliano nchini.
Amesema uwepo wa vitendea kazi hivyo utarahisisha mafundi kuwafikia wateja kwa haraka zaidi na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa na shirika hilo.
Cecil amesema idara ya ufundi imejipanga kuhakikisha vitendea kazi hivyo vinatumika ipasavyo ili kuleta tija kwa shirika na wateja wake.
Amesema pia TTCL inalenga kuwafikia wateja wengi zaidi katika mikoa mbalimbali nchini na kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano.
Katika hatua nyingine, amesema shirika hilo lina dhamira ya kuunganisha wateja milioni moja ndani ya kipindi cha miaka mitatu kupitia maboresho ya huduma zake.
Amesema mafanikio hayo yanaendana na azma ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za mawasiliano kwa wakati na kwa ufanisi zaidi.



